Wataka kujua upelelezi kesi ya ATCL utakamilika lini

Tuesday April 9 2019

By Pamela Chilongola,Mwananchi. [email protected]

Dar es salaam. Upande wa utetezi wameutaka upande wa mashtaka kuieleza  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni lini upelelezi utakamilika katika kesi inayowakabili mawakala 10 wa Shirika la Ndege Tanzania(ATCL).

Mawakala hao wanakabiliwa na makosa matatu likiwemo la utakatishaji fedha na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh10,874,280 kwa lengo la kuwakatia watu tiketi za ndege za shirika hilo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali,Janeth Magoho kuieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

 

Wakili wa upande wa utetezi, Augustine Kulwa amedai kuwa upande wa mashtaka wamekuwa wakija na kauli ya kudai upelelezi haujakamilika na imeshapita zaidi ya miezi mitatu jambo ambalo wateja wake wanaendelea kusota rumande huku wakikosa haki zao za msingi.

Kulwa alidai kuwa kutokana na kauli inayotolewa mara kwa mara  na upande wa mashtaka wakidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, ameiomba mahakama hiyo iwape onyo.

"Kati ya washtakiwa hao mmoja ana mtoto wa miezi mitatu hadi minne na huyo mtoto yupo mahabusu kama naye mtuhumiwa ambapo ni kinyume na sheria ya mtoto sura ya 21 ya mwaka 2009, inakataza asipelekwe jela hata kama ikiwa ni mahabusu, "alidai Kulwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu Salum Ally, amesema upande wa mashtaka wafuatilie upelelezi umefikia wapi ili shauri hilo liweze kuendelea.

Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23,2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Fabian Ishengoma, Adamu Kamara, Marlon Masubo, Alexander Malongo, Tunu Kiluvya, Jobu Mkumbwa, Mohamed Issa, Godfrey Mgomela, Absalom Nyusi na Janeth Lubega.

Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matatu ambayo ni ya kulisababishia hasara shirika hilo, kutumia njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh10,874,280.

Advertisement