Wataka mifuko mbadala kugawiwa bure

Muktasari:

  • Ikiwa ni siku ya kwanza ya matumizi ya mifuko mbadala baada ya kupigwa marufuku mifuko ya plastiki wafanyabiashara waomba mifuko hiyo kugawiwa bure

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa soko la Kinondoni Mtambani wameiomba Serikali kutengenza mifuko mbadala watakayoweza kuigawa bure kwa wateja.

Ombi hilo limetolewa leo Jumamosi Juni mosi, 2019 ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kutumika kwa mifuko mbadala baada ya Serikili kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

Wakizungumza na Mwananchi Digital wafanyabiashara hao wamesema mifuko  iliyotolewa huwezi kumpa mteja bure kutokana na bei yake.

Stanslaus Kobero muuzaji wa nafaka sokoni hapo, amesema wateja wengi walishazoea kwenda sokoni bila mfuko anaponunua vitu unamwekea kwenye mfuko na kuondoka.

"Mifuko iliyotolewa bei iko juu nanunua mifuko 20 kwa Sh800 hadi 1,000 anapokuja mteja inabidi kumuuzia Sh200 anapokosa hana mfuko au fedha inabidi kuondoka," amesema Kobelo.

Amesema ipo haja ya Serikali kutengeneza mifuko itakayouzwa kwa bei nafuu ambayo wafanyabiashara wataweza kuwapa  wateja bure.

Mfanyabiashara wa mbogamboga, Selina Leon amesema  gharama ya mifuko mipya iko juu na walishazoea kuwawekea wateja mboga kwenye mifuko lakini kwa sasa inabidi kuwasokotea kwenye gazeti.

"Tulikuwa tunanunua mifuko Sh700 pakiti nzima unatumia kwa siku tatu kwa kuwawekea wateja mboga lakini hii inauzwa 250 hadi 300 na ukishachafuka haufai," amesema Selina.

Ameongeza kuwa ipo haja ya Serikali kubuni mifuko ya bei rahisi ambayo wateja watapewa bila kutozwa gharama yoyote kwani wakati mwingine wanapokosa mfuko hawanunui.