Watalii 5,412 walitembelea kisiwa cha Mafia mwaka 2018

Muktasari:

Kisiwa cha Mafia ni moja ya maeneo ya kimkakati nchini Tanzania katika  uendelezaji wa utalii wa fukwe. Siku za hivi karibuni kisiwa hicho kimekuwa kikitembelewa kwa wingi na wageni kutoka ndani na nje ya nchi

Dodoma. Watalii 5,412 wametembelea kisiwa cha Mafia  mwaka 2017/18 sawa na ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na watalii 4,817 waliokitembelea mwaka 2016/17.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Juni 18, 2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu wakati akijibu swali la mbunge wa Mafia (CCM), Mbaraka Dau aliyetaka kujua idadi ya watalii waliotembelea kisiwa hicho mwaka 2017/18.

Katika majibu yake Kanyasu amesema kati ya watalii hao Watanzania walikuwa  252, kwamba Serikali inaendelea  na mikakati ya kuboresha miundombinu ya kisiwa hicho ikiwa ni pamoja na kujenga meli na kuboresha maegesho ya meli katika bandari ya Nyamisati na Mafia.

Baadhi ya vivutio vilivyopo katika kisiwa hicho ni Papa Potwe, magofu ya kale, utamaduni wa fukwe, michezo ya kwenye maji na kuogelea na samaki aina ya papa.