Watano mbaroni kwa kupiga ramli chonganishi

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbrod Mutafungwa akionesha kifaa walichokuwa wakitumia waganga wa kienyeji maarufu rambaramba (pichani) kupiga ramli chonganishi na kutoa mapembe kwenye nyumba za watu eneo la chamwino manispaa ya Morogoro.  Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia waganga watano wa kienyeji kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi

Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia waganga watano wa kienyeji kwa tuhuma za kupiga ramli chonganishi.

Mbali na kuwakamata, polisi wamezuia jaribio la ndugu kuwahamisha wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya rufaa mkoani Morogoro kuwapeleka kwa waganga hao.

Akizungumza leo Alhamisi Julai 11, 2019 kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Willbrod Mutafungwa amewataja kuwa ni Idd Mpuye maarufu Dk Makata,  Athumani Ramadhani  maarufu Dk Simba, Chande Rajabu (mtoto wa Simba),  Mussa Kombo (Mchinja) na  Seif Lindoi maarufu Dk Kipara, wote wakazi wa Dar es Salaam.

Amesema waganga hao walikuwa wakipiga ramli chonganishi na kutoa majini kwenye nyumba za wakazi wa kata ya Chamwino kwa Sh 5000 kila nyumba huku wakidai kuna mapembe yaliyowekwa na majirani au ndugu.

“Tulipopata taarifa tulifika  katika maeneo hayo na kukuta makundi ya watu yakiwafuatilia waganga hao ili waone mapembe yanayotolewa kwenye nyumba za watu kitendo ambacho kinahatarisha amani baina ya majirani na ndugu,” amesema kamanda huyo.

Amesema waganga hao  walipopekuliwa walikutwa na matunguli, vioo, mtambo unaoonesha sura za wachawi, dawa mbalimbali pamoja na Sh231,000, noti mbili za zamani na fedha ya Zambia Kwacha 1,000.

Wakihojiwa na waandishi wa habari waganga hao wamesema kuwa utaalamu wao wa kutoa mapembe wamerithi kwa wazazi wao na wamekuwa wakiyatoa kwa wachawi na  wanaowekewa na wachawi kwa kutumia vifaa maalumu, pia wanatibu magonjwa mbalimbali, kusafisha nyota na kuondoa mikosi.

Hata hivyo,  walikiri kutokuwa na vibali vya kufanya kazi hiyo huku wakibaisha kuwa wenyeviti wa Serikali za mitaa wanajua ujio wao.