Watanzania waitwa kutafiti mgogoro wa Israel, Palestina

Muktasari:

Balozi wa Palestina nchini, amesema utafiti huo utasadia kuijua historia ya Mashariki ya Kati ambayo mtafiti wa mambo ya kale Dk Uri Davis anasema imekuwa ikipotoshwa kwa maslahi ya Marekani

Dar es Salaam. Ubalozi wa Palestina nchini umewakaribisha Watanzania kufanya tafiti zaidi kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati ili kujua ukweli wa historia kati ya Israel na Palestina.

Wito huo umetolewa na balozi wa Palestina nchini, Hamdi Mansour AbuAli ameyasema hayo leo Februari 21, 2019 wakati akimtambulisha mtafiti wa mambo ya kale, Dk Uri Davis ambaye ana asili ya Israel lakini amekuwa akitetea haki za Wapalestina.

"Ubalozi wetu utakuwa wazi kushirikiana na Watanzania iwapo watataka kufanya tafiti kuhusu historia ya Mashariki ya Kati, yupo mtaalamu wetu wa mambo ya kale ambaye atasaidia katika hilo," amesema balozi huyo.

Balozi AbuAli amesema mtaalamu huyo amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu huko Israel hasa Wapalestina wanaoishi huko.

Kwa upande wake, Dk Davis amesema ukweli kuhusu historia ya Mashariki ya Kati umekuwa ukipotoshwa kwa maslahi ya Marekani bila kujali ukiukwaji wa haki za binadamu katika ukanda huo.

Amesema bado kuna fursa kubwa ya kufanyika kwa tafiti zitakazoongeza uelewa kwa watu mbalimbali duniani. Amesema pamoja na tofauti zao za kihistoria, bado haki za binadamu ni muhimu kuheshimiwa na pande zote mbili.