Watanzania wang’ara tuzo za kimataifa za kuhifadhi Quran

Muktasari:

  • Kijana  Zakaria Sheha Ally ameibuka mshindi katika fainali ya tuzo ya kimataifa ya kuhifadhi Quran zilizofanyika leo Dar es Salaam likihusisha nchi kumi kutoka Bara la Afrika, Ulaya na Asia.

Dar es Salaam. Kijana  Zakaria Sheha Ally (16), amewatoa kimasomaso Watanzania baada ya kuibuka kidedea katika fainali ya tuzo ya kimataifa ya kuhifadhi Quran zilizofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini hapa.

Fainali hizo zimefanyika leo, Jumapili  Mei 26, 2019. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa rais mstaafu, Mohammed Gharib Bilal na Mufti mkuu Sheikh Aboubakar Zubeir walihudhuria.

Nafasi ya pili katika fainali hizo ilinyakuliwa na Gaffari Mohammed  (14), anayetokea Uingereza, wakati  Shamsi Mwalimu Saidi (19) kutoka Zanzibar akishika nafasi ya tatu.

Kutokana na taratibu wa mashindano hayo ulioshirikisha nchini 10 kutoka mabara matatu (Asia, Afrika na Ulaya), Mshindi wa kwanza amepata zawadi ya Sh11.5milioni,  Mshindi wa pili Sh9.2milioni na Mshindi wa tatu Sh6.9 milioni.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ally amesema siri kubwa ya kuibuka mshindi ni jitihada za kuhifadhi kitabu hicho ambapo alitumia muda wa miaka saba.