VIDEO: Watanzania watakiwa kujiandaa kikamilifu soko la SADC

Monday August 5 2019

By Kelvin Matandiko, Mwananchi, [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax amewataka wafanyabiashara nchini Tanzania kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuanza kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika nchi wanachama.

Dk Stergomena ambaye ni Mtanzania ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa katika wiki ya Viwanda kwa Nchi 16 za SADC. Uzinduzi huo umefanywa na Rais John Magufuli katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) nchini Tanzania.

Katika hotuba yake, Dk Stergomena amewataka wafanyabiashara kutoa taarifa katika wizara ya viwanda pale wanapokutana na vikwazo wakati wa shughuli zao za kibiashara ndani ya jumuiya hiyo iliyoondoa vikwazo na baadhi ya tozo za kibiashara.

“Huu ni mwanzo tu, kutakuwa na vikao 60 vitakavyofanyika nchini, kwa hiyo tutumie fursa zilizopo, kuna fursa za huduma , miundombinu na nyingine nyingi,”  amesema.

Chimbuko la wiki ya Viwanda ya SADC linatokana na maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Aprili 29, 2015  mjini Harare, Zimbabwe.

Katika hotuba yake, amepongeza juhudi za utekelezaji wa miradi ya umeme na miundombinu ya barabara ikiwamo reli na barabara, zinazofanywa na serikali ya Tanzania ambazo zinaonyesha matumaini ya kukabiliana na changamoto.

Advertisement

Kwa mujibu wa SADC, Mkakati wa Viwanda wa SADC una lengo la kuongeza kasi ya kuimarisha ushirikiano na ushindani  wa kiuchumi kutoka katika nchi zisizokuwa wanachama wa SADC.

Advertisement