Watanzania watakiwa kushiriki kongamano la wajasiriamali

Muktasari:

Siku mbili kabla ya kufanyika kongamano la kimataifa la ujasiriamali na maendeleo ya biashara ndogo Afrika (ICAESB), mkuu wa idara ya masoko wa shule kuu ya bishara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omari Mbura amesema bado kuna fursa ya  wazawa kushiriki

Dar es Salaam. Siku mbili kabla ya kufanyika kongamano la kimataifa la ujasiriamali na maendeleo ya biashara ndogo Afrika (ICAESB), mkuu wa idara ya masoko wa shule kuu ya bishara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omari Mbura amesema bado kuna fursa ya  wazawa kushiriki.

Kongamano hilo  la 19 lililoandaliwa na UDBS litafanyika Agosti 15 na 16, 2019  likilenga kukuza biashara nchini.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni ' ujasiriamali wa kiafrika katika utandawazi', litatoa fursa  kwa Watanzania kutangaza biashara zao na kuuza nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 13, 2019 kuhusu maendeleo ya kongamano hilo,  Dk Mbura amesema maandalizi ni mazuri.

“Chuo Kikuu Dar es Salaam ni cha wananchi kila mmoja anakaribishwa kushiriki kwenye kongamano hili la kipekee la ujasiriamali kikubwa wafuate utaratibu tu.”

“Takribani washiriki 120 kutoka mataifa 10  yakiwemo Sweden, Nigeria, Uingereza, Afirika Kusini, Kenya, Marekani na Botswana," amesema Dk Mbura.

Amesema kongamano hilo litagawanywa katika maeneo matatu ili kutoa fursa kwa washiriki na miongoni mwa mada zitakazozungumzwa ni  biashara na viwanda, ukuaji shirikishi wa bishara na mafuta, gesi na madini.

Dk Mbura anafafanua kuwa kongamano hilo litakwenda sambamba na maadhimisho ya kusherehekea miaka 40 tangu kuanzishwa kwa UDBS.

Julai 30, 2019 mratibu msaidizi wa kongamano hilo, Dk Winnie Ngumi amewaeleza wanahabari kuwa kongamano hilo linafanyika kila mara na limesaidia  kuboresha ufundishaji katika masomo ya biashara.