Watanzania watakiwa kuzidisha maombi ili Mungu asikie mvua inyeshe

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir

Muktasari:

  •  Waislamu nchini wamefanya ibada maalumu ya kuombea mvua kutokana na ukame unaoendelea maeneo mbalimbali nchini. Wametakiwa kuzidisha maombi ili Mwenyezi Mungu asikie dua zao na kuleta mvua ya neema.

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuzidisha maombi ili Mwenyezi Mungu asikie kilio chao na kuleta mvua ya neema itakayorutubisha mazao mashambani.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Machi 24, 2019 na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir wakati wa dua maalumu ya kuomba mvua iliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mufti amesema Quran inaelekeza kwamba kunapotokea ukame katika nchi, watu wamlilie Mungu ili arekebishe hali. Amewataka Watanzania kuzidisha dua ili siku zijazo mvua ya neema inyeshe katika maeneo mbalimbali nchini.

"Tumetoa agizo nchi nzima kwamba shughuli kama hii ya kuomba mvua ifanyike. Masheikh na maimamu waendelee kuomba mvua kila mara kwenye hotuba na dua zao. Waumini pia wasichoke, hili ni jambo letu sote," amesema Mufti.

Kiongozi huyo amesema anaamini mvua ya neema itanyesha katika kipindi kifupi kijacho.

Amewataka Watanzania waendelee kumwomba Mungu afanye wepesi katika jambo hilo.

Awali, akitoa mawaidha kwenye ibada hiyo, Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga amesema ukame uliopo sasa unatokana na maovu ya Watanzania, hivyo amewataka wamrudie Mola wao ili arudishe neema ya mvua.

"Ukame tulionao sasa ni kwa sababu ya madhambi yetu. Majanga yote, ukata wote unatokana na yale tunayoyafanya kwa mikono yetu. Maombi kama haya ndiyo yatakayotuinua," amesema Chizenga.

Amesema Watanzania hawana budi kuomba kwa kasi ili wapate msamaha na mvua ishuke. Amesema Mungu ni mwingi wa kusamehe, amesikia maombi ya watoto wake.

Baadhi ya waumini waliohudhuria swala hiyo wamesema wameguswa kwa sababu mvua ni muhimu si tu kwa wakulima bali kwa kila kiumbe kinachoishi duaniani.

"Siku hizi kuna joto kali sana, lakini mvua ikinyesha linapungua. Kwa hiyo, mvua inamgusa kila mmoja wetu, tufanye lile tuliloelekezwa na viongozi wetu, yaani tuzidishe maombi," amesema Omary Twaha.