Watoto milioni tatu wapatiwa vyeti vya kuzaliwa

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (Rita), Emmy Hudon

Muktasari:

  • Serikali imeanzisha utaratibu wa watoto kusajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa kwenye ofisi za kata, zahanati na vituo vya afya tofauti na zamani usajili ulikuwa ukifanyika kwenye ofisi za mkuu wa wilaya pekee

Singida.  Zaidi ya watoto milioni tatu wameandikishwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa kwenye mikoa 13 nchini Tanzania kupitia kampeni maalum ya kuwasajili watoto walio chini ya umri wa miaka mitano inayoendelea.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni hiyo mkoani Singida,  kaimu mkurugenzi mtendaji wa wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (Rita), Emmy Hudon amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anasajiliwa na kupewa cheti ndani ya muda mfupi.

Amesema kampeni hiyo inayofadhiliwa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), kampuni ya simu za mkononi ya Tigo na ubalozi wa Canada nchini imepangwa kufika mikoa yote nchini ili kurahisisha utoaji wa vyeti hivyo.

“Kwa sasa watoto wengi hawajasajiliwa hivyo kupitia kampeni hii kila mtoto atapata huduma karibu kabisa na kwenye makazi yake,” amesema.

Mwakilishi mkazi wa Unicef nchini, Maniza Zaman amesema ni haki ya kila mtoto kusajiliwa na kutambuliwa katika nchi yake.

Amesema shirika hilo linalofanya kazi kwenye mataifa zaidi ya 150 litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anasajiliwa na kupewa cheti cha kuzaliwa.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi amesema tayari zaidi ya watoto 45,000 wameandikishwa katika mkoa huo tangu kuanza kwa uandikishaji huo siku tano zilizopita.

“Nataka niseme hivi, watoto wote wa Singida lazima waandikishwe, niwaombe viongozi wa dini, wanasiasa na kila mmoja kuhamasisha jambo hili, uandikishwaji huu ni bure kabisa,” amesema.