Watoto walivyonusurika kutekwa Dar es Salaam

Sunday February 10 2019

By Jackline Masinde, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watoto wa familia moja ya meneja mkuu wa Chuo Kikuu cha Agha Khan, Gamariel Mboya wamenusurika kutekwa na watu wasiojulikana Jumatano iliyopita nyumbani kwao eneo la Kisarawe Two Upanga jijini Dar es Salaam.

Watoto hao, Jemima Mboya (8), Jeffrey Mboya (5) na Jansen Mboya (3) ni wanafunzi wa Shule ya Joyland International iliyopo Mikwembe Toangoma.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Temeke, Awadhi Haji jana alisema taarifa hizo wanazisikia tu kwenye mitandao na wamejaribu kufuatilia na kubaini hazijaripotiwa kwenye kituo chochote cha polisi.

Hata hivyo, Mboya ambaye ni baba wa watoto hao alilieleza Mwananchi kuwa aliripoti tukio hilo kituo kidogo cha polisi Kibada lakini hakupewa RB namba na badala yake alipewa namba za dharura za kituo hicho.

“Nilipewa namba nikaambiwa ikitokea taarifa yoyote niwajulishe huku wakinisihi kuwa makini zaidi,” alisema.

Mwananchi lilichukua namba za dharula za kituo hicho cha polisi na kuwapigia, ambapo askari aliyepokea simu alimuunganisha mwandishi na mkuu wa upelelezi Kigamboni aliyejitambulisha kwa jina la Walelo.

Mkuu huyo wa upelelezi alimweleza mwandishi kuwa taarifa hizo zina utata na kuomba apatiwe namba ya wazazi wa watoto hao ili aweze kuzungumza nao kwani wanaweza kuwasaidia kuwapa taarifa nzuri zaidi.

Jinsi mpango ulivyokwama

Taarifa kutoka kwa wazazi wa watoto hao zinaeleza kuwa walikwenda watu wawili nyumbani kwao wakiwa na gari nyeusi na kumtaka dada wa kazi, Julieth Seth (18) kuwapatia watoto ili wawapeleke shule kwa madai basi la shule limeharibika.

Akielezea mkasa huo, Seth alisema: “Ilikuja gari ndogo nyeusi ikiwa na watu wawili, mmoja alikuwa kijana ambaye nilimtambua kwa sura kwani aliwahi kuja nyumbani akiulizia nyumbani kwa Juma siku mbili kabla na mtu mzima ambaye sikumtambua,”alisema.

Seth alisema watu hao walianza kumlazimisha kuwatoa watoto ili waende shule kwa walichoeleza wametumwa na mama yao. “Niliwaeleza kuwa watoto wamekwenda shule lakini bado hawakunielewa na badala yake walianza kunitisha, niliingia ndani na kufunga mlango.”

Mboya alisema inaonekana watu hao walikuwa na mpango wa kuteka watoto wake na walikuwa na mtu wa karibu anayeitambua vema familia yake aliyekuwa akiwapa taarifa ya kinachoendelea.

Advertisement