Watu 26 wafa kwa ebola siku moja DRC

Muktasari:

  • Ni kufuatia mlipuko wa pili wa ugonjwa huo ambao umeing’ang’ania nchi hiyo kwa muda mrefu sasa

Kinshasa. Watu 26 wamethibitishwa kufa ndani ya siku moja kwenye jimbo la Kivu Kaskazini kutokana na maradhi ya ugonjwa wa ebola unaoendelea kusumbua nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mlipuko wa sasa ni wa pili na ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa baada ya ule uliokumba maeneo ya Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014-2016 na kuua watu zaidi ya 11,000.

Wizara ya Afya nchini DRC imethibitisha vifo vya watu 957 huku ikirekodi visa vya watu 891 ambao wana maambukizi ya ugonjwa huo.

Serikali imetangaza mikakati zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa maambukizi zaidi kama anavyoeleza Daktari Jean Jacques Muyambo, aliyenukuliwa na Redio ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI).

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa ebola mashariki mwa DRC yameendelea kuwa sugu kutokana na makundi ya waasi kushambulia vituo vya afya vinavyotoa matibabu.