Watu 500,000 kulipwa fidia kupisha ujenzi Mto Msimbazi

Muktasari:

  • Benki ya Dunia (WB) wamekubali kutoa fedha kiasi cha Dola 100 milioni kinachosubiriwa ni Wizara ya Fedha kuidhinisha, kwa ajili ya upanuzi wa Mto Msimbazi.

Dar es salaam. Wakazi zaidi ya 500,000 wanatarajia kulipwa fidia kupisha mradi wa ujenzi wa Mto Msimbazi ili kuepusha madhara yanayotokea wakati wa mvua.

Hayo yamesemwa leo Aprili 26,2019 na Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua madhara yanayotokea kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa Mto Msimbazi pindi mvua zinaponyesha.

Amesema endapo mradi huo utafanikiwa utakuwa ni suluhisho la kudumu kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa mto huo.

"Wizara ya ofisi ya Raisi Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) tayari wameshatafuta suluhisho la kudumu ikiwa ni kuomba mkopo wa Dola 100 milioni (zaidi ya Sh 2.2 bilioni) wenye masharti nafuu Benki ya Dunia kwa ajili ya kulipa fidia,” amesema Mtulia.

Amesema tayari Benki ya Dunia imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu kinachosubiriwa ni Wizara ya Fedha kuidhinisha.

"Benki ya Dunia wamekubali kutoa fedha kiasi cha dola 100 milioni kinachosubiriwa ni Wizara ya Fedha kuidhinisha," amesema mbunge huyo.

Amesema mradi huo wa kudumu ukifanikiwa katika bonde hilo kutakuwa na sehemu nzuri za kupumzikia.

Naye mkazi wa Kigogo, Ramadhani Yahaya amesema mvua zimekuwa zikileta madhara makubwa ikiwemo kukosa sehemu ya kuishi.

"Mvua zimekuwa zikituathiri sana, mwaka 2011 wakati wa mvua nyumba saba ziliondoka na maji na kwa sasa mvua zinaponyesha tunalazimika kuhama makazi," amesema Yahaya.