Watu 60 hufa kila siku Tanzania kwa matumizi ya mkaa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba 

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba  ametoa takwimu za vifo vinavyotokana na matumizi ya mkaa kuwa watu 60 hufa kila siku Tanzania na 22,000 kwa mwaka  

 


Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amesema watu 22,000 hufa hapa nchini kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya mkaa na kuni.

Waziri Makamba ameyasema hayo kwenye mdahalo wa Jukwaa la Fikra linaloendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na ITV na Redio One unaofanyika leo Alhamisi Februari 7, 2019 kwenye ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Amesema kwamba kila siku hapa nchini hufa watu 60 kutokana na athari za mkaa.

Waziri huyo amesema kutokana na athari hizo Mwananchi imekuja na jambo jema litakaloonyesha mwanga wa mwelekeo wa matumizi ya nishati hiyo.

Amesema jamii inajitetea kuwa mkaa ni rahisi, lakini ukichunguza zaidi mkaa ni gharama kuliko nishati nyingine.

Makamba amefafanua bei ya mkaa inaonekana kuwa chini kama inavyosemwa kwa sababu gharama inayohesabiwa ni utayarishaji na usafirishaji ukiacha magogo yanayotumika.

"Iwapo gharama ya magogo na utayarishaji zingejumlishwa mkaa ungekuwa ghali pengine kuliko nishati nyingine," amesema na kuongeza.

"Ili kudhibiti matumizi haya, haihitaji kukata wala kuupiga rungu, bali ni kujumlisha gharama zake kuanzia gogo na utayarishaji wake bila shaka kila mmoja atataka kutumia nishati mbadala," amesema.

Amefafanua kuwa wakifanya hivyo kuna dhana kuwa wanawadhulumu masikini, lakini hao masikini watanufaika kwa muda baadaye hawatapata hiyo nishati na wataishi kwenye umasikini mkubwa.

Amesema kutokana na uharibifu wa misitu unaofanyika hapa nchini, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakuwa lakini utajiri wa nchi unashuka na ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa ukataji wa misitu.

"Mwananchi hongereni kwa hiki mlichokifanya kwa sababu pamoja na kuandika habari zenu pia mnatuleta pamoja kujadili masuala mbalimbali ya jamii, suala la mkaa ni mtambuka na kuja na wazo hili ni ujasiri mkubwa," amesema Makamba.