Watu 9 wanusurika ajali ya ndege Mafia

Muktasari:

  • Watu Tisa wamesurika kifo baada ya ndege ya kampuni ya Tropical kuanguka katika Uwanja wa Ndege wa Mafia mkoani Pwani wakati inaruka.

Dar es Salaam. Watu Tisa wamesurika kifo baada ya ndege ya Kampuni ya Tropical iliyokuwa inaruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Mafia mkoani Pwani kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) nchini Tanzania kuanguka.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumanne Agosti 6, 2019, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga amesema watu sita kati ya Tisa waliokuwa kwenye ndege hiyo wamejeruhiwa.

“Ni kweli ndege ya shirika la Tropical Air Zanzibar imeanguka Mafia majira ya saa nne leo asubuhi (Agusti 06, 2019) na ilikuwa kwenye safari zake za kawaida kutoka Uwanja wa Ndege wa Mafia kwenda Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na ilikuwa ina abiria Tisa na hakuna abiria ambaye amefariki lakini kuna majeruhi sita,” amesema Kamanda Lyanga na kuongeza; “Bado tunaendelea kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vinavyohusika kujua chanzo cha ajali hiyo ni nini.”

Kamanda Lyanga amesema abiria wote waliweza kutoka kabla ya ndege hiyo kuwaka moto na kuteketeza mali zilizokuwa kwenye ndege hiyo.

“Mali zote ambazo zilikuwa kwenye ndege hiyo ambazo thamani yake bado haijajulikana zimeteketea pamoja na ndege yenyewe imeungua sehemu kubwa,” amesema kamanda huyo.

Amesema majeruhi Sita wamepelekwa katika Hospitali ya Mafia kwa matibabu.