Watu sita wajeruhiwa kwa silaha za jadi Arusha

Mmoja wa majeruhi katika mgogoro wa kugombea mipaka Kati ya kijiji cha Lendikinya na Emairete wilayani Monduli mkoani Arusha, Tingidosoto Sima (60) mkazi wa kijiji cha Lendikinya kata ya Sepeko akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Monduli akipatiwa matibabu. Picha na Happy Lazaro

Muktasari:

  • Watu sita wamejeruhiwa vibaya baada ya kuibuka mgogoro wa kugombea mipaka kati ya vijiji viwili vilivyopo wilayani Monduli mkoani Arusha

Arusha. Watu sita wamejeruhiwa vibaya kwa silaha za jadi baada ya kuwepo kwa mgogoro wa kugombania ardhi kati ya vijiji viwili vilivyopo wilayani Monduli mkoani Arusha.
Mgogoro huo umekuwapo muda mrefu ukihusisha vijiji vitatu vya Lendikinya, Emairete na Arkalia ambapo wananchi wa vijiji hivyo wanagombea mipaka kati ya msitu wa hifadhi ya Lendikinya. Hata hivyo kwa sasa mgogoro huo umepamba moto ukihusisha vijiji viwili vya Lendikinya na Emairete.
Akizungumzia tukio hilo jana usiku Jumamosi Machi 30, 2019, daktari wa zamu katika hospitali ya wilaya Monduli, Debora Karega alisema Machi 28,2019 alipokea majeruhi sita katika hospitali hiyo.

Alisema kati ya hao mmoja ameruhusiwa na wengine wawili wamehamishiwa hospitali ya mkoa Arusha ya Mount Meru kutokana na hali zao kutokuwa nzuri.
"Ni kweli tumepokea majeruhi sita wakiwa na majeraha mbalimbali katika sehemu za kichwani, mikononi na miguuni kutokana na kupigwa kwa sime, mishale na fimbo.”

“Wawili hali zao si nzuri, tumewahamisha kwa ajili ya kwenda kuchekiwa zaidi katika hospitali ya mkoa kutokana na kuumia zaidi maeneo ya kichwani," alisema Karega.
Mmoja wa majeruhi waliolazwa hospitali ya wilaya ya Monduli, Tingidosoto Sima (60) kutoka kijiji cha Lendikinya kata ya Sepeko alisema akiwa na wazee wenzake walikwenda eneo hilo kuzungumza na wananchi hao wa vijiji hivyo vya Lendikinya na Emairete.

Alisema walishangaa kuona wanaanza kushambuliwa na wananchi wa kijiji Emairete bila hata kuelewa sababu za kufanya hivyo.  
Majeruhi mwingine, Lekishoy Mbasia mkazi wa Lendikinya alisema wananchi hao waliwashambulia kwa mapanga, sime, mishale na mawe bila hata kujali wao ni wazee kitendo ambacho kimewaumiza sana.

Aliomba Serikali iingilie kati mgogoro huo kwani kwa sasa unaelekea katika hatua mbaya hadi kupelekea watu kutaka kuuana.

Kufuatia tukio hilo, baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Monduli mkoani Arusha limesitisha shughuli zote za kilimo zilizokuwa zikifanyika katika vijijiji hivyo hadi hapo muafaka utakapopatikana.

Mwenyekiti  wa halmashauri ya wilaya ya Monduli, Isack Joseph aliyasema hayo jana jioni wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika wilayani humo. 

Alisema baraza kwa pamoja wamefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa mipaka kwa muda mrefu kati ya msitu wa hifadhi ya Lendikinya na vijiji hivyo ambavyo vinazunguka msitu huo.
"Mkurugenzi naomba uwaandikie barua watendaji wa maeneo hayo kuhusu kusitishwa shughuli mbalimbali katika vijiji hivyo hadi tutakapofikia muafaka na tutatembelea eneo hilo kuhakikisha tunapata hati zote za vijiji hivyo,” alisema.

"Tumeshangaa kukamatwa kwa diwani Sumuni wa kata ya Monduli juu, akituhumiwa kuhusika na vurugu hizo, wakati yeye ndiye aliyekuwa mtoa taarifa kuhusu tukio hilo, huo ni uonevu mkubwa maana kama ni kukamatwa kwa nini asikamatwe na diwani wa kata hiyo nyingine," alisema Isack. 

Mbunge wa Monduli  (CCM), Julius Kalanga alisema bado hawajaridhika  na utatuzi huo wa migogoro mbalimbali katika wilaya hiyo, hivyo kuwataka viongozi kila mmoja kwa nafasi yake kutekeleza wajibu wake kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika kwa kuzungumza na wananchi hao kwa karibu
Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Arusha, James Manyama alithibitisha kutokea tukio hilo na kuwa watu wanne  wanashikiliwa akiwemo diwani Sumuni.

Aliongeza kwamba vurugu hizo ziliwahi kutokea mara ya kwanza ambako kamati ya ulinzi na usalama ilisuluhisha na hii ni mara ya pili kutokea tena na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.