Watu wachache wanahudumiwa na mtandao wa majitaka nchini

Muktasari:

  • Maeneo mengi ya uswahilini yamejaa uchafu kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kuuondoa kwa wakati

Dodoma. Msimu wa mvua unaoendelea baadhi ya maeneo nchini ni fursa kwa baadhi ya watu kuzibua vyoo na kuruhusu uchafu usombwe na maji kuelekea mabondeni.

Ni kipindi ambacho maradhi ya mlipuko kama kipindipindu na magonjwa ya tumbo hukithiri. Ingawa wengi wanachukizwa na utaratibu huu lakini hakuna namna.

Bunge limesema ni watu 511,208 pekee wanaohudumiwa na mtandao wa majitaka kwenye miji 11 ambayo ni Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora, Moshi, Tanga, Songea na Iringa. Kwa hesabu za haraka haraka ni chini ya wastani wa watu 50,000 kutoka kila mji.

Hata Dar es Salaam yenye zaidi ya watu milioni tano walio kwenye mtandao wa majitaka ni wachche kiasi hicho.

Umeshawaza watu hao watakuwa wanapatikana mitaa ipi? Kilimanjaro yote ni Moshi pekee kama ilivyo kwa Songea mkoani Ruvuma, waliobaki hawana pa kwenda.

Kwa kuona upungufu huo, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeishauri Serikali kuongeza kasi ya kutekeleza mipango na miradi ya mbalimbali ya majitaka na usafi wa mazingira.

Ushauri huo umetolewa jana Alhamisi Mei 2, 2019 mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa, alipowasilisha taarifa kwenye mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji iliyotoa hoja ya kutaka Bunge liridhie matumizi ya Sh634.19 bilioni.

“Uchambuzi wa kamati umebaini huduma ya ufanisi wa mazingira kwa upande wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira mjini hutolewa kwa njia ya uondoshaji wa majitaka pekee. Kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na mtandao huo, majitaka huondolewa na magari maalumu na kumwagwa kwenye mabwawa ya majitaka,” amesema Mgimwa.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema majitaka yanaiongezea Serikali gharama za matibabu kutokana na magonjwa yanayoibuka