Watu wanane wafungwa maisha kwa kuchoma moto kituo cha polisi

Kituo cha Polisi Bunju A kilichochomwa moto na washtakiwa ambao wamehukumiwa kifungo cha Maisha Jela

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa imewahukumu kifungo cha maisha gerezani washtakiwa wanane kati ya 18 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuchoma moto kituo cha Polisi cha Bunju A jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewahukumu kifungo cha maisha jela washitakiwa wanane baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju A jijini Dar es Salaam huku wengine 10 wakiachiwa huru.

Jumla ya washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa 35, awali Mahakama ilikwishawaachia huru 17 na kubaki 18 ambapo wanane ndio wametiwa hatiani leo Ijumaa Februari 23, 2019 huku 10 wakiachiwa huru.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa sita ikiwemo kuchoma kituo hicho moto Julai 10 mwaka 2015.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amesema kitendo walichofanya washitakiwa ni unyama kwa kuchoma moto kituo hicho.

"Kitendo hiki ni cha kinyama, hakiwezi kuvumilika na sioni sababu ya kuwaonea huruma kwa kuwa walihatarisha usalama wa nchi," amesema Simba.