Watuhumiwa 56 wa makosa mbalimbali wakiwamo waganga wa kienyeji washikiliwa Mwanza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne  Muliro akionyesha kwa waandishi wa habari wa mkoa huo Nyara za serikali zilizokamatwa  wakati wa Zoezi la Operesheni dhidi ya waganga wanaopiga Ramli chonganishi.picha na Johari Shani

Muktasari:

 

  • Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 56 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali wakiwamo waamiaji haramu na waganga wa kienyeji.

Mwanza. Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watuhumiwa 56 wa matukio mbalimbali wakiwamo wahamiaji haramu na waganga wa ramli chonganishi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, kamanda wa polisi mkoa huo, Jumanne Murilo amesema katika tukio la kwanza wamekamata wahamiaji haramu 19 raia wa Ethiopia waliokutwa nyumba ya kupanga mtaa wa Amani kata ya Butimba jijini Mwanza.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa jana saa 5.00 asubuhi kwenye chumba alichopanga mkazi wa mtaa wa Mkuyuni ikiwa ni siku tatu toka achukue chumba hicho.

"Jeshi la polisi linaendelea kuwashikilia na watafikishwa katika idara ya uhamiaji kwa ajili ya  hatua nyingine za kisheria," amesema  Muliro.

Katika tukio jingine, polisi wamewakamata waganga wa kienyeji 15 wanaopiga ramli chonganishi, kati yao wakiume sita na wa kike 10 wakiwa na nyara za Serikali.

Kamanda Muliro alizitaja nyara hizo kuwa ni,  mikia miwili ya nyumbu, magamba ya chatu, vipande vya  mayai ya mbuni, pembe za  wanyamapori,  mafuta ya simba, ngozi ya kenge na vipande vinne vya  ngozi vya wanyamapori aina tofauti.

Mbali na tukio hilo pia polisi wamekamata watuhumiwa 11 kati yao mmoja mwanamke wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye ujazo wa kilogramu mbili na gramu 762 na mirungi kilo 10.

Kamanda Muliro pia amewaeleza waandishi wa habari kuwa wamekamata pombe uliyokuwa imehifadhiwa kwenye viroba vya konyangi pakiti 14 pamoja na  mtuhumiwa mmoja eneo la Nyegezi  pamoja na maji ya betri fake dumu mmoja lenye  ujazo wa lita 15 na chupa  228 zenye ujazo wa lita moja.

Wakati huohuo, polisi wamekamata watuhumiwa sugu nane pamoja na mwalimu mmoja aliyempa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mwamboku na anashikiliwa kwa kitendo hicho.