Watumiaji bahari watakiwa kuvuta subira

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), jana iliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maafa yanayoweza kusababishwa na kimbunga Kenneth, huku ikiwasihi watumiaji wa bahari kuvuta subira.

Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema kuwa kimbunga hicho kilikuwa kinaendelea kusogea katika pwani ya Kusini kikielekea Msumbiji.

Akizungumza na kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), Dk Kijazi alisema hadi jioni kimbunga hicho kilikuwa katika eneo la wastani wa kilomita 200 kutoka maeneo ya pwani ya Tanzania.

“Kimbunga hiki tayari kimeongezeka nguvu kwa maana ya ukubwa, kina kilomita 140 kwa saa na awali tulisema kilomita 130,” alisema.

Alisema mgandamizo mdogo wa hali ya hewa katikati ya kimbunga hicho ulikuwa unaendelea kuongezeka kidogo hadi jioni.

“Hali halisi inaonyesha kwamba kimbunga hiki kinavuta mawingu mengi kutoka Magharibi kwa hiyo kwa usiku wa leo (jana kuamkia leo) tutarajie kuwa kutakuwa na mvua katika maeneo mengi ya nchi.”

Mbali na mikoa ya Kusini, aliwataka wananchi wa maeneo mengine kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na mvua zilizotarajiwa kunyesha usiku. “Upepo bado ni mkali na tunatarajia kufikia kesho (leo) kimbunga kitakuwa kimetua Msumbiji na upepo utafikia kilomita 100 kwa saa na kilomita hizo ni nyingi kwa sababu zinaweza kusababisha uharibifu.”

Alisema kitakapotua huko kinaweza kusababisha madhara kwa mikoa ya Kusini na kuwataka watumiaji wa bahari kusitisha shughuli kwenye eneo hilo ili kuepuka madhara.

Dk Kijazi aliwataka wavuvi na watumiaji wengine wa bahari kuwa na subira mpaka kimbunga hicho kitakapopunguza mgandamizo wake.

“Tukifikia mahali mgandamizo wa hali ya hewa ukiwa hauleti madhara watu wanaweza kuingia baharini,” alisema Dk Kijazi.