Watumiaji holela wa dawa za nguvu za kiume hatarini

Muktasari:

  • Wataalam wa afya wanasema kwamba utumiaji wa dawa za nguvu za kiume bila ushauri wa wataalam wa afya unaweza kuongeza tatizo badala ya kulipunguza kwa sababu chanzo cha tatizo wanakuwa hawajakiondoa na wakati mwingine hawakijui.

Dar es Salaam. Matumizi ya dawa mbalimbali za kutibu tatizo la nguvu za kiume bila ushauri wa daktari, yameelezwa kuchochea zaidi upungufu wa nguvu hizo kwa watumiaji walio wengi kinyume na matarajio yao.

Wataalamu wa afya wamesema tabia ya unywaji wa dawa mbalimbali ikiwamo Viagra na kuvamia kila kitu kinachodaiwa kuongeza nguvu hizo, ni kichocheo kikubwa cha kuzimaliza kabisa.

Daktari kutoka Kituo cha Elimu na Tiba, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Shindo Kilawa alisema matumizi hayo yamewafanya wanaume wengi kupoteza kwa kiwango kikubwa uwezo wao licha ya kuwa tatizo lao lingetibiwa kirahisi na wataalamu wa afya.

Alisema wengi wanatumia dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya wakiamini wanajitibu.

“Wanaweza kuongeza tatizo badala ya kupunguza kwa sababu chanzo cha tatizo wanakuwa hawajakiondoa na hiyo ni kwa sababu hawajajua chanzo, bali wanatumia zile dawa ili kuongeza tu uwezo wa kusimamisha uume,” alisema Dk Kilawa.

Alisema ni vyema kuonana na wataalamu wa afya pale wanapogundua kupungukiwa nguvu za kiume kwa ushauri na namna nzuri ya kurudisha nguvu zao na uwezo wa kuzalisha mbegu pale inapobidi.

“Wanaume wanapaswa kuacha matumizi ya pombe, sigara na kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika vizuri. Wajiepushe na tabia hatarishi zinazoweza kumletea magonjwa ya zinaa na mengine yanayoweza kuathiri mifumo hiyo ya uzalishaji.

“Lakini pia magonjwa kama kisukari, presha ya kupanda na mengine hupunguza uwezo wa nguvu za kiume na kupunguza uwezo wa kuzalisha mbegu za kiume zenye nguvu na zenye afya.”

Alisema madhara hayo hayaishii katika nguvu za kiume pekee, bali huweza kusababisha hitilafu katika uwezo wa mbegu za kiume kuzalisha.

“Upungufu wa mbegu za kiume kitaalamu tunaita ‘Oligospermia’ na mbegu kutokuwepo kabisa inaitwa ‘azoospermia’,” alisema.

Alisema suala la kutengeneza mbegu za kiume huratibiwa na mfumo wa fahamu, mfumo wa homoni na mfumo wa uzazi kwa ujumla. Alisema ili mwanamume azalishe mbegu zinazofaa, ni lazima mifumo hii ifanye kazi kwa karibu.

Dk Kilawa alisema ikiwa moja ya mfumo huo utaathiriwa kwa namna yoyote ile, uzalishaji wa mbegu za kiume huweza kupungua au kutokuwapo kabisa.

Alisema kukosa nguvu za kiume na kuathiri uzalishaji wa mbegu kwa wingi pia husababishwa na unene na vitambi, msongo wa mawazo, joto kali hasa sehemu za uume.

Tafiti kidunia

Wataalamu wametahadharisha kwamba ubora wa mbegu za kiume miongoni mwa wanadamu umekuwa ukishuka kwa kiasi kikubwa, na kuathiri uzazi.

Wataalamu wanaamini unene pamoja na mtindo wa maisha siku hizi wa kuketi vipindi virefu bila kufanya mazoezi unachangia, pamoja na mabadiliko kwenye lishe.

Matokeo ya utafiti huo yaliyowasilishwa katika kongamano la kila mwaka la Chama cha Matibabu ya Uzazi Marekani ambalo linaendelea mjini Denver, Colorado, yanaonyesha athari kwenye kiasi cha mbegu za uzazi anazotoa mwanamume na ubora na uwezo wa kuogelea katika majimaji ukeni.

Utafiti huo ulishirikisha wanaume 124,000 waliotembelea kliniki za uzazi Ulaya na Marekani na kubainika kwamba ubora wa mbegu za uzazi unashuka kwa asilimia mbili kila mwaka.

Wanaume waliotafuta usaidizi kutungisha mimba waliongezeka kutoka 8,000 hadi 60,000 katika kipindi cha mwaka 2002 hadi 2017.

Kiwango cha wanawake walioomba huduma ya kutumia teknolojia kutungisha yai mbegu (IVF) kutokana na kasoro kwa waume zao pia kinaongezeka.

Mwandishi mwenza wa ripoti ya matokeo hayo ya utafiti James Hotaling alisema: “Kuna uwezekano wa wanaume wengi kuwa wagumba na hilo linazua wasiwasi.”