Watumiaji simu wapewa angalizo

Muktasari:

  • Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) limewataka watumiaji wa simu kuwa makini na  taarifa potofu zinazosambazwa juu ya usajili mpya wa laini za simu.

Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu usajili mpya wa laini za simu ukiendelea kushika kasi, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) limewataka watumiaji wa simu za mkononi kutafuta taarifa sahihi kutoka mamlaka husika na kupuuzia taarifa potofu zinazosambazwa kwenye mitandao.

Miongoni mwa taarifa zinazozungumziwa ni kuwa ifikapo Mei Mosi mwaka huu kama mtu hajasajili laini kwa alama za vidole fedha zilizo kwenye simu yake zitafungiwa.

Pia baraza hilo limefafanua kuwa usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole utaanza Mei Mosi na sio kumalizika siku hiyo.

Katibu mtendaji wa TCRA- CCC, Mary Msuya leo amesema mitandaoni kumekuwapo na taarifa za upotoshaji kuhusu usajili huo na kusababisha usumbufu kwa watumiaji.

“Kumekuwapo na taarifa kuwa tarehe 1/5/2019 ni siku ya mwisho ya usajili wa laini za simu  kwa kutumia salama za vidole na kuwa ifikapo tarehe hiyo laini zisizosajiliwa zitafungwa  hii  taarifa hiyo sio sahihi.

“Usajili mpya wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole utaanza tarehe 1/5/2019 na sio mwisho wa zoezi hilo kama baadhi ya taarifa zisizo sahihi zinavyoeleza,”  amesema.

Kuhusu fedha zilizopo mitandaoni kufungiwa, Msuya amesema hakuna uhusiano ingawa ni muhimu kufanya usajili huo.

Suala hilo pia lilitolewa ufafanuzi bungeni na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Atashasta Nditiye aliyeeleza kuwa Serikali ndiyo imetoa maelekezo ya usajili wa simu vya alama za vidole.

Alisema njia hiyo itawezesha kutambua nani anatumia namba gani na akashauri watumiaji kuwa na laini moja kwa mtandao mmoja.

Msuya pia ametaka watumiaji wa huduma za mawasiliano kufuatilia taarifa kutoka mamlaka husika ambazo zimethibitishwa ili kuepuka kupokea na kusambaza taarifa zisizo sahihi na kuleta mkanganyiko kwa jamii.

“Tunawashauri watumiaji wa huduma za mawasiliano kutumia fursa hii ya usajili wa laini kwa mfumo wa alama za vidole kama ilivyoelekezwa na mamlaka ya mawasiliano kwa faida ya watumiaji na taifa kwa ujumla,” amesema.