Watumishi 10,899 Serikali za mitaa hawajapandishwa vyeo, kuongezwa mishahara

Thursday April 11 2019

 

By George Njogopa, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  imebaini watumishi 10,899 katika mamlaka za Serikali za mitaa 17 hawajaidhinishwa upandishwaji wa vyeo na ongezeko la mishahara.

Ripoti hiyo inasema hali hiyo inaweza kuathiri utendaji kazi wa mamlaka za Serikali za mitaa na hivyo kuzorotesha juhudi za Serikali za kuleta maendeleo.

Ripoti hiyo ambayo imewekwa hadharani na CAG, Profesa Mussa Assad jana inaonyesha pia mamlaka za Serikali za Mitaa 41 hazijawasilisha makato ya mishahara kwa taasisi husika yenye jumla ya Sh.1,048,170,313.

Mapungufu mengine kama yalivyobainishwa na ripoti hiyo ni kuwapo kwa watumishi 491 wanaokaimu nafasi za ukuu wa vitengo katika mamlaka za Serikali za mitaa 129 kwa zaidi ya miezi sita ambao hadi sasa bado hawajaidhinishwa.

“Pamoja na hayo pia tumebainia mambo mengine kadhaa kama vile kuwapo kwa nafasi za wazi 74 katika mamlaka ya Serikali za mitaa 20, upungufu wa watumishi 149,943 katika mamlaka za Serikali za mitaa 158, kutohamisha taarifa za mishahara za watumishi 13,090 katika mamlaka za Serikali za mitaa 33 waliohamishiwa katika taasisi nyingine za Serikali,” amesema Assad.

Ikigusia tathmini ya usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, ukaguzi wa CAG umebaini udhaifu katika halmashauri nyingi ambao imesema unahitaji kushughulikiwa.

Advertisement

Baadhi ya mambo muhimu yaliyoonekana katika eneo hilo ni pamoja na malipo ya Sh. 6,716,649,510 yakiwa na nyaraka pungufu katika mamlaka za Serikali za mitaa 106 .

“Pia tumebaini kuwapo kwa hati za malipo zenye jumla ya Sh. 1,672,467,823 katika mamlaka za Serikali za mitaa 17 ambazo hazikuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi na matumizi yasiyokuwa na tija yenye juma ya Sh.720,206,743 yamefanyika katika mamlaka za Serikali za mitaa 20,” inasema.

Aidha ripoti hiyo imebaini kuwa, magari, mitambo na pikipiki 504 katika mamlaka za Serikali za mitaa 97 yamekaa muda mrefu bila kutumika na dawa zenye thamani ya Sh 276,887,999 ziko katika stoo za halmashauri sita  kwa vipindi mbalimbali kuanzia mwaka 1990 hadi 2018 bila kuteketezwa.

Zaidi ya hayo, ripoti hiyo inasema mamlaka za Serikali za mitaa zimethaminisha ardhi na kuzijumuisha katika taarifa zao za fedha bila kufanya jitihada za kupata hati za umiliki wa ardhi.

Advertisement