Wawekezaji wakutana Dar, wajadili kuanzisha viwanda Tanzania

Washiriki wa mkutano wa kimataifa wa wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba wakifuatilia mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekutana kwenye mkutano wa kujadili namna ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba kwa ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP) nchini Tanzania

Dar es Salaam. Wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekutana kwenye mkutano wa kujadili namna ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba kwa ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP) nchini Tanzania.

Mkutano huo unaoendeshwa kwa ushirikiano baina Bohari ya Dawa (MSD) na PPP unatokana na takwimu za 2016 zinazoonyesha asilimia 85 ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi huagizwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumza na wawekezaji hao leo Jumatano Julai 17, 2019 jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwe amesema Serikali inaandaa mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuondoa baadhi ya kero zilizokuwa zinakwamisha suala hilo.

“Niwahakikishie mpo eneo sahihi, Tanzania ni nchi sahihi kwa uwekezaji na tayari kero 54 zilizokuwa zinakwamisha uwekezaji zimeondolewa katika bajeti ya 2019/2020,” amesema Bashingwa.

Amewataka wawekezaji kufanya uamuzi wa kubaki nchini na kuwataka kutumia mkutano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) utakaoshirikisha zaidi ya watu 1,000 kuonyesha viwanda vyao.

Amesema anatamani kuona Tanzania inakuwa mzalishaji mkubwa wa dawa na vifaa tiba vitakavyotosheleza mahitaji ya soko la ndani, nchi za SADC.

Awali Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu  amesema waliibua wazo la uanzishwaji viwanda hivyo ili kuondokana na utegemezi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Katika ujenzi huo wa viwanda, Bwanakunu amesema imeshauriwa kiwanda cha Pamba kijengwe Mwanza, kiwanda cha maji-tiba kijengwe mkoani Mbeya na Kiwanda cha dawa kijengwe mkoani Pwani.

Kwa upande wake Kamishna wa PPP katika Wizara ya Fedha, Dk John Mboya amesema licha ya kumaliza tatizo la dawa, uanzishwaji wa viwanda hivyo utasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuajiri zaidi ya watu 800.