Wawili kizimbani kwa dawa za kulevya

Tuesday June 25 2019

 

By Daniel Francis, Sifras Kingamkono, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watu wawili wakazi wa Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 567.4

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Hamisi Hassan Mfinanga (44) Mkazi wa Chang'ombe na Ramadhani Musa Kibabani mkazi wa Chang'ombe.

Akiwasomea shtaka linalowakabili wakili wa Serikali, Jenipher Masue alidai kuwa washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya Juni 8,2019 eneo la Kariakoo wilaya ya Ilala, kinyume cha Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, kifungu cha 15,1(a).

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote, kwakuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za uhujumu uchumi  isipokuwa Mahakama Kuu divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Kama Mahakama ya Ufisadi.

Masue alidai kuwa  upelelezi wa shtaka hilo bado haujakamilika hivyo aliiomba Mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Augustina Mmbando, baada ya kusikiliza maelezo hayo aliweza kuahirisha kesi hiyo Hadi Julai 8, 2019 itakapotajwa na watuhumiwa kupelekwa rumande.

Advertisement

Advertisement