Wazazi, walezi wakumbushwa kuzungumza na watoto wao

Wednesday May 15 2019

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wazazi na walezi wamekumbushwa kuitumia siku ya familia duniani kuzungumza na watoto wao hasa vijana ili wajue vikwazo vinavyowafanya washindwe kufikia ndoto zao.

Wakati dunia ikisherehekea siku ya familia leo, matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji, ubakaji, ndoa na mimba za utotoni yanaendelea kuripotiwa licha ya kuwapo kampeni mbalimbali za kupinga na kutokomeza vitendo hivyo.

Mkuu wa Idara ya Jinsia, afya ya uzazi na makundi maalum kutoka shirika la Plan International, Katanta Simwanza amesema wazazi na walezi wapo kimya na hawana nafasi na kuzungumza na watoto wao.

Akizungumza wakati wa mdahalo wa vijana juu ya usawa wa kijinsia uvyoweza kuchochea maendeleo leo Mei 14, Katanta amesema ulinzi wa watoto lazima uanzie kwenye familia.

"Unaweza kuwalinda watoto kama utakuwa na muda wa kuzungumza nao, leo tuanze kuzungumza na watoto wetu," amesema Katanta.

Awali mchambuzi wa masuala la kijinsia Richard Mabala alisema lazima jamii na Serikali wahakikishe watoto wa kike na kiume wapo salama.

"Hata huko shuleni sio salama kwa sababu baadhi ya walimu wanawatongoza wanafunzi wa kike lakini pia njiani sio salama pia, tuongeze ulinzi," amesema Mabala.

 Mabala amesema bado mfumo dume unaendelea kuwadumaza wasichana.

"Kwa mfano msichana akishapata mimba anaitwa mama jina la kijana linaondoka lakini mvulana hata anae watoto 75 kama hajafikia miaka 35 hadi 45 anaitwa kijana, hapa hakuna usawa," anasema Mabala.

Mwenyekiti wa vijana kutoka Plan International Neema Ole Ndemlo anasema ukatili wa kijinsia utaisha ikiwa vijana watafikishiwa elimu sahihi na kujitambua.

Mabala amesema ili msichana aweze kusema naweza lazima aandaliwe mazingira wezeshi kuanzia ngazi ya familia.

Advertisement