Wazazi wa Azory Gwanda wamlilia Rais Magufuli

Wazazi wa Azori Gwanda, mwandishi wa habari wa Mwananchi aliyepotea Kibiti mkoani Pwani mwaka 2017 wakiwa nyumbani kijiji cha Msimba kata ya Mungonya wilaya ya Kigoma. Kushoto ni Obadia Gwanda na Eva Mpulumba. Picha na Anthony Kayanda.

Muktasari:

Kutokana na kukosa misaada kutoka kwa mtoto wao, wazazi wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications,  Azory Gwanda aliyepotea mwaka 2017, wamemuomba Rais John Magufuli aagize vyombo vya dola kufanya upelelezi wa kina ili kujua hatma yake.

Kigoma. Wazazi na ndugu wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda aliyetekwa na watu wasiojulikana wamemuomba Rais John Magufuli kuagiza vyombo vya Dola kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama yupo hai au amekufa.

Azory ambaye kituo chake cha kazi kilikuwa mkoani Pwani alichukuliwa na watu hao Novemba 21, 2017.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti, sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara, na kumchukua.

 

Watu hao walimpeleka hadi shambani ambako mkewe alikuwa akilima na akamuaga kuwa anaenda kazini, lakini hajarudi hadi leo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne Mei 21, 2019 katika kijiji cha Msimba, kata ya Mungonya Wilaya ya Kigoma mama mzazi wa mwanahabari huyo, Eva Mpulumba (85) amesema mtoto wao alikuwa tegemeo kwa kuwasaidia mahitaji muhimu ya chakula na gharama za matibabu.

 

"Tunaishi maisha ya shida na ufukara mkubwa tangu Azori alipotoweka, familia haina msaada na hatujui kama yupo hai au alikufa, tunaomba Rais (John Magufuli) atusaidie mtoto wetu apatikane," amesema Eva.

 

Hata hivyo baba mzazi wa Azory, Obadia Gwanda (96) alishindwa kuzungumza kutokana na umri mkubwa.

 

John Gwanda, mdogo wake Azory amesema wameamua kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kuona ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu ndugu yake alipopotea na hakuna taarifa zozote juu yake.

 

"Sisi kama familia hapa Kigoma tunaomba Serikali yetu ambayo ni sikivu kwa wananchi wake, Rais (John Magufuli) atusaidie ni jinsi gani kaka yetu atapatikana kwa kutumia vyombo vyake vya dola kufanya upelelezi," amesema John.

 

"Kama bado yupo hai apatikane na kama alikwishafariki basi tujue ili wazazi wafanye wanavyojua kwa ajili ya msiba kwa sababu lazima msiba utandikwe," amesema John.

 

John anasema amebaki na jukumu la kuwatunza wazazi wao pamoja na kusaidia mahitaji mengine kwa familia ya Azory  iliyopo Kibiti mkoani Pwani kwa kugharamia mahitaji ya shule na chakula kwa watoto.

 

Baadhi ya majirani wamesema kupotea kwa Azory kumewapa simanzi kwa vile alikuwa kijana mwenye tabia njema kwa jamii na aliheshimika kwao.

Mikael Kasunzu,  ameiomba Serikali kufanya upelelezi wa kina ili kuhakikisha anapatikana akiwa hai na arejee katika shughuli zake za kila siku.

Naye Prisca Kavakule amesema familia ya Gwanda haina msaada kwa sasa na wamebaki kuwa tegemezi na ombaomba kwa watu na mitaani kwa ajili ya kujipatia kipato cha kugharamia mahitaji yao ya chakula.