Waziri Bashungwa aanza kutema cheche

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa amesema si jambo zuri kila jambo kutolewa maelezo na Rais John Magufuli, kuwataka watumishi wa wizara hiyo kujituma na si kusubiri kutumwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi.

 


Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ameeleza jinsi anavyokerwa na watu wanaosubiri mambo yakwame waanze kukimbizana na utekelezaji wa mambo mbalimbali.

Bashungwa aliyeteuliwa kuongoza wizara hiyo siku nne  zilizopita kuchukua nafasi ya Joseph Kakunda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais John Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 12, 2019 wakati akikaribishwa ofisini na watumishi wa wizara hiyo jijini Dodoma.

Amesema kitendo cha Rais Magufuli  kutaja baadhi ya viwanda visivyofanya kazi ni changamoto wanayotakiwa kuifanyia kazi kwa kujituma badala ya kusubiri kutumwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi.

“Tukiwa tunasubiri hadi kuwe na tukio pale Ikulu Rais aguse wizara yako hilo si jambo zuri. Kwa viwanda vilivyobinafsishwa, vinavyofanya kazi lazima tuwe na kipimo cha kujua ufanyaji kazi wake,” amesema Bashungwa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa naibu Waziri wa Kilimo.