Waziri Bashungwa kuapishwa kesho

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeelezea kuwa kufuatia uteuzi uliofanyika jana wa mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri uliohusisha pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), viongozi wapya wataapishwa kesho saa 8:00 mchana.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli kesho anatarajia kuwaapisha viongozi wapya Ikulu jijini Dar es Salaam, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Rais Magufuli alimteua Innocent Bashungwa, kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara jana Juni 8, akichukua nafasi ya Joseph Kakunda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu iliyotolewa leo Jumapili Juni 9, 2019 imeeleza kuwa Bashungwa ataapishwa kesho sambamba na Katibu Tawala wa mkoa wa Njombe, Charles Kichere na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dk Edwin Mhede.

Baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Magufuli atashuhudia tukio la kampuni ya Bharti Airtel International kutoa mchango wa Dola za Marekani milioni 1 sawa na Sh2.270 bilioni.

Fedha hizo zinatolewa ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo huku Sh3 bilioni zinazotokana na malipo ya Sh1 biloni kila mwezi kwa serikali ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanywa kati ya Serikali ya Tanzania na Bhati Airtel International kuhusu umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

“Matukio haya yataanza saa 8:00 mchana na kurushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya Youtube channel ya Ikulu (Ikulumawasiliano).” Imesema taarifa hiyo.