Waziri Biteko aagiza watumishi wasimamishwe haraka

Muktasari:

  • Waziri wa Madini Dotto Biteko ameagiza kusimamishwa kazi na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watumi

Dodoma. Waziri wa Madini, Doto Biteko amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila kuwasimamisha na kuwachukulia hatua za kinidhamu mara moja watumishi watatu wa wizara hiyo kwa kuhusika kugawa leseni za uchimbaji wa madini bila kufuata utaratibu.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 18, 2019 na waandishi wa habari jijini Dodoma, Biteko amesema watumishi hao walihusika kugawa eneo la wachimbaji wadogo Malela  Morogoro bila kufuata utaratibu wa utoaji wa leseni katika maeneo hayo kwa mujibu wa kanuni 17 (3) ya Kanuni za Madini za Mwaka 2018.

Amewataja watumishi hao wanaotakiwa kusimamishwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

 “Kuna baadhi ya maeneo yalitengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ikiwemo eneo la Malela Demacrated Area Morogoro, yametolewa bila kufuata taratibu za utoaji leseni katika maeneo hayo kama zilivyoainishwa Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Madini za mwaka 2018,”amesema.

Amesema haiwezekani Serikali itenge maeneo kwa wachimbaji wadogo wao wakafanye wanavyojisikia kwa tamaa zao na kwamba hatawavumilia watumishi kama hao.

Aidha Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoainishwa na kutangazwa  na Serikali kwa ajili ya wachimbaji wadogo (Dermacated areas) yaliyotolewa leseni za uchimbaji mdogo tu kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.

Amesema kwa mujibu wa kanuni hiyo, maeneo hayo hayatakiwi kutolewa leseni za uchimbaji wa kati wala mkubwa ili kuwaendeleza na kuimarisha kiuchumi wachimbaji wadogo.