Waziri Hasunga atishia kuifuta NFRA

Thursday March 14 2019Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga  

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Japhet Hasunga ametishia kuufuta Wakala wa Chakula nchini (NFRA) kama hawataweza kujirekebisha na kununua mazao ya wakulima kwa wingi.

Hasunga ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 14, 2019 alipotembelea NFRA Jijini Dodoma alipokwenda kuzindua mashine maalum ya kusafisha mahindi ambayo ilitolewa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

Waziri amesema NFRA wamejikita katika uhifadhi wa mahindi pekee wakati wanatakiwa kununua, kuhifadhi na kutafuta masoko ya kuuza.

Amesema mazao ya wakulima zaidi ya tani tano bado yako mikononi mwa wakulima wakati NFRA wangekuwa wametafuta masoko nje hadi sasa wangeshauza na kununua.

“Mnaweza kuniambia sababu za kwa nini mnashindwa kununua tani laki tano kwa wakulima…nyie kazi yenu si kuhifadhi tu, bali mlitakiwa kununua na kuuza pia katika masoko mengine duniani,” amesema Hasunga.

Amewataka watumishi wa NFRA kujitathmini na kutumia mbinu za kuwasaidia wakulima vinginevyo watakuwa wameshindwa kufikia malengo.

Kingine Hasunga ameagiza yajengwe maghala ya kisasa yenye kuhifadhi chakula hata kwa miaka mitano lengo ni kufikia miaka 10 au 15 kama ilivyo kwa Marekani ambao wanahifadhi miaka hiyo wakati Tanzania mazao yakifika miaka 2 au mitatu yanaharibika.

Advertisement