Waziri Jaffo awasifu WB kwa kuboresha miji Tanzania

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jaffo akihutubia madiwani, watendaji wa kata na mitaa, wenyeviti wa mitaa na wafanya biashara (hawapo pichani) mjini Kigoma wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa kukusanya mapato (LGRCIS) na taarifa ya kijiografia (GIS). Picha na Anthony Kayanda.

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Tamisemi, Seleman Jaffo ameishukuru Benki ya Dunia (WB) kwa kutoa mkopo nafuu wa zaidi ya Sh2 trilioni kugharamia miradi ya maendeleo nchini Tanzania

Kigoma. Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jaffo ameIshukuru Benki ya Dunia (WB) kwa kutoa fedha ya kugharamia uboreshaji wa majiji, manispaa na miji hapa nchini.

Akizungumza na madiwani, watendaji wa mitaa na kata, wenyeviti wa mitaa, wafanyabiashara, viongozi na baadhi ya wakazi wa Kigoma mjini leo Ijumaa Machi 15, 2019, Waziri Jaffo amesema mkopo huo umeimarisha miundombinu na kuboresha mazingira.

Benki ya dunia imetoa fedha ya ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara, vituo vya mabasi na madampo ya takataka ikiwa ni mkopo nafuu.

"Katika miji yetu sasa taa za barabarani zinawaka usiku, kuna mitambo ya kuzoa taka ngumu, barabara zinajengwa na master plan (mpangilio) ya miji yetu inaandaliwa kisasa ili kuondoa tatizo la makazi holela," amesema Jaffo.

Mradi wa kuboresha majiji ya Tanga, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Arusha pamoja na manispaa za Kigoma Ujiji, Mtwara Mikindani na Ilemela umegharimu zaidi ya Sh900 bilioni tangu ulipoanza mwaka 2012.

Jaffo ametaja mradi wa kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es salaam kuwa unagharimu Sh660 bilioni ambapo mradi mwingine unaohusisha manispaa na miji 18 nchini utagharimu zaidi ya Sh520 bilioni.

Ameomba wananchi kutoa ushirikiano na kulinda miradi hiyo kwa vile licha ya kuifanya miji kupendeza, pia inaboresha mazingira.

Mtaalamu wa mipango miji kutoka Benki ya Dunia, MaryGrace Lugakingira amesema asilimia 70 ya miji yote nchini haijapangwa kitaalamu.

"Matokeo yake ndio maana Serikali imekuwa ikilazimika kuvunja nyumba za watu ili kupisha ujenzi wa barabara na miradi mingine ya Serikali," amesema Lugakingira.

Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava ameiomba Serikali iendelee kuutazama kipekee mkoa wa Kigoma kwa vile kuna changamoto nyingi za maendeleo.