Waziri Jafo: Bajeti 2019/2020 inajibu matatizo ya Watanzania

Tuesday June 25 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amesema bajeti ya mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni ni ya watu kwa sababu inakwenda kutekeleza miradi ya miundombinu.

Jafo amesema leo Jumanne Juni 25, 2019 wakati akijibu hoja za wabunge walizotoa katika mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni ambayo tayari imepitishwa na Bunge la Tanzania.

Jafo amesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni Sh284.7 bilioni na kwamba kwa imani yao watafanya mabadiliko makubwa.

Amesema pia Mfuko wa Barabara unaangalia mgawanyo wa fedha wa asilimia 30 kwa 70 lengo likiwa ni kuhudumia barabara zilizopo chini ya Tarura nchini.

Kwa upande wa afya, Jafo amesema ukiachia mbali ujenzi wa vituo vya afya 352  mwaka huu wa fedha 2019/2020 wanajenga vituo vya afya 52 na kuendelea na ujenzi wa hospitali 67 na wana ujenzi wa hospitali mpya 27.

“Kwa hiyo utaona katika mpango wa miaka miwili ni hospitali 94 ni outstanding performance kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania ambalo hili tunakila namna ya kujifunza kama tangu uhuru tulikuwa na hospitali 77 pekee yake ,”amesema.

Advertisement

Amesema baadhi ya wabunge walikuwa wakisema bajeti hiyo inajali vitu lakini ukweli ni bajeti hiyo inajali watu.

Amesema katika hospitali walizozijenga kila hospitali wataalam waajiriwa sio chini ya 20 na kwamba ukipiga hesabu unaona jinsi gani watu wanaenda kuguswa na ajira.

“Ukisema bajeti hii ni vitu hapana, bajeti hii ni ya watu inakwenda kwenye kutekeleza miundombinu na inaenda kugusa watu wengine,” amesema.


Advertisement