Waziri Jafo: Vijana wafundishwe nyimbo za uzalendo

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania, Selemani Jafo

Muktasari:

  • Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amesema katika ziara zake zote atakazofanya jambo la kwanza ni kusikiliza wanafunzi wakiimba wimbo wote wa Taifa bila kukosea.

Mtwara. Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania, Selemani Jafo ameagiza wakuu wa shule, maofisa elimu na maofisa utamaduni kusimamia maagizo ya Serikali kuhakikisha wanafunzi wanajua kuimba nyimbo za uzalendo wa Taifa, Tanzania Tanzania na tazama ramani.

Akifunga mashindano ya Umishumta yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi kutoka mikoa 24 nchini, hivi karibuni, Waziri Jafo alisema katika ziara zake atakazofanya jambo la kwanza kabla hajafanya chochote atataka kusikiliza nyimbo hizo zikiimbwa na vijana na kwamba sio jambo la hiari.

“Hili jambo sio hiari ni maagizo mnapaswa kwenda kulisimamia, hatutaki kuona vijana ambao wanapoteza hata uzalendo wao hawajui hata kuimba wimbo wao wa Taifa, tutengeneze utaifa wetu, tutengeneze uzalendo wetu kama Taifa, imani yangu jambo hili litaleta faraja,” alisema Jafo

Mmoja wa wanafunzi, Ally Isihak alisema mara nyingi wanapokuwa shulei wamekuwa wakiimba beti mbili za wimbo wa Taifa na hivyo kusababisha wengine kushindwa kuimba.

“Shuleni kwetu tunaimba wimbo wa Mungu Ibariki Afrika na Ibariki Tanzania tu huo mwingine aliosema waziri wa Tanzania Tanzania na Tazama ramani hatuujui ila tukifundishwa tutaweza kuimba,” alisema Isihaka.

Katika mashindano hayo ya Umishumta mkoa wa Tabora umeibuka mshindi wa jumla.