Waziri Jafo ataka mweka hazina Iringa kuchunguzwa kwa ubadhirifu

Muktasari:

  • Waziri wa nchi ofisi ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo leo amezungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kuagiza mweka hazina wa manispaa ya Iringa kuchunguzwa kwa tuhuma za ubadhirifu uliotokea akiwa Bahi jijini Dodoma kisha kuhamishwa kituo cha kazi

Dodoma. Waziri wa nchi ofisi ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo ametoa wiki moja kwa mweka hazina wa manispaa ya Iringa, Saad Ishabairo kuchunguzwa akidai utendaji wake una mashaka.

Waziri Jafo amemtaka mweka hazina huyo kuchunguzwa wakati Iringa iliongoza kwa makusanyo ya mapato ya ndani kwa manispaa zote nchini katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mapato 2018/19.

Hata hivyo, mweka hazina huyo anachunguzwa kutokana na makosa ya ubadhirifu wa fedha uliotokea akiwa halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kisha kuhamishiwa Iringa.

"Huwezi kufanya makosa sehemu moja unakimbilia mahali pengine ukidhani utakuwa salama,  halipo hilo,  naagiza uchunguzi ufanyike ndani ya siku saba na akibainika hatua zichukuliwe," amesema Jafo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma

Alidai Ishabairo na aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Rachel Chuwa walishindwa kusimamia vema fedha za mradi wa elimu wa ‘Equity’ ambazo halmashauri hiyo ilipoteza mamilioni ya fedha.

Katika hatua nyingine, Jafo amemwagiza naibu waziri wake, Mwita Waitara kuwa mkali katika miradi ya elimu na asicheke na wazembe agizo ambalo Mwita amesema atafanya hivyo lakini si kwa kumuonea mtu.