Waziri Jafo awataka vijana Tanzania kupambana na adui roho mbaya

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Selemani Jafo

Muktasari:

Vijana 500 wamekutana jijini Dodoma nchini Tanzania kwenye kongamano la siku ya kimataifa ya vijana ambapo pamoja na mambo mengine mada mbalimbali zitawasilishwa.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Selemani Jafo amewataka vijana kuungana na kupambana na adui roho mbaya ili wapendane.

Jafo ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 15, 2019 wakati akiwahutubia vijana katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana.

“Vijana ni watu wa ajabu lakini sio wote wanaona vijana wenzao wametengeneza bidhaa nzuri lakini anaacha anakwenda kununua nyingine ya nje,” amesema.

Amesema wana ajenda moja kubwa tuungane kwa pamoja kupambana na adui mmoja roho mbaya na kwamba wako ambao wako tayari kuwakatisha tamaa wenzao.

“Vijana kwanza tupendane, upendo ndio iwe ajenda kubwa sana ya sisi vijana. Acheni kurembaremba fanyeni kazi ya kusaidia Watanzania wenzetu,” amesema.

Meneja Programu na Maendeleo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNPFA) Dk Majaliwa Marwa amesema jumla ya vijana 500 kutoka maeneo mbalimbali nchini walikutana ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa.