Waziri Kairuki awapa neno wafanyabiashara wanawake

Monday June 17 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji, Angella Kairuki amesema Serikali inakusudia kutengeneza sheria ambayo itasimamia mazingira bora ya biashara nchini kama yalivyobainishwa kwenye mwongozo wa kuboresha mazingira ya biashara (Blue Print).

Kairuki ameyasema hayo leo Juni 17 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la wafanyabiashara wanawake kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) linalofanyika kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wanawake katika biashara.

Amesema Oktoba au Novemba, Serikali itakuja na muswada wa kuboresha mazingira ya biashara na kila sekta itatoa mapendekezo yake ili sheria hiyo itatue na kusimamia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini.

"Nanyi wanawake kupitia TPSF mtoe mawazo yenu ili yapelekwe kwenye kikosi kazi cha kupunguza kodi," amesema Waziri Kairuki na kuongeza kuwa bajeti ya serikali ya mwaka huu imeondoa kodi 54.

Waziri huyo amesema Julai 2019, Serikali itaanza rasmi kuitekeleza Blueprint. Hata hivyo, amesema tayari Taasisi nyingine za Serikali zimeanza kutekeleza ikiwamo suala la kupunguza kodi.

Awali, Mwakilishi wa wanawake wazalishaji katika Bodi ya TPSF, Fatuma Kange amesema wafanyabiashara wanawake wamedhamiria kutengeneza mabilionea 20 kati ya 100 ambao Rais John Magufuli alisema analenga kuwatengeneza kwenye utawala wake.

Advertisement

“Leo tumekutana hapa ili kujiwekea mikakati ya kufikia malengo hayo. Tutaangalia fursa mbalimbali za biashara kwa wanawake, kama kuna haja tutaiomba serikali ituondolee kodi wakati wa kuagiza na kuuza bidhaa zetu nje ya nchi,” amesema Kange.

Mwakilishi wa chama cha wafanyabiashara wanawake wa Kigoma, Doroth Takwe amesema pasipoti za muda wanazotumia kuvuka mipaka ya nchi zinawagharimu fedha nyingi kwa sababu wanatakiwa kuihuisha kila siku wanapovuka mpaka kuingia nchi nyingine.

Takwe ameiomba Serikali iwatengenezee vitambulisho maalumu ambavyo watavitumia kwa miezi mitatu mpaka sita. Alisema wako tayari kulipia vitambulisho hivyo kwa sababu vitapunguza usumbufu na gharama kubwa wakati wa biashara zao.

Advertisement