MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Waziri Kambona akutana na balozi wa Marekani-8

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi Marekani ilivyoanza kukatishwa tamaa na Uingereza kutokana na kutofanya haraka juhudi za kutekeleza mpango wa kuivamia Zanzibar. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, David Dean Rusk aliandika telegramu kwa waziri mwenzake wa Uingereza kuonyesha hilo na kwamba Marekani, ingeweza kufanya yenyewe. Wakati hayo yakiendelea meli za Marekani zilionekana Pwani ya Afrika Mashariki na Abdulrahman Mohammed Babu alitishika.

Kadiri Wamarekani walivyojitahidi kuwasisitiza Waingereza waongeze kasi yao ya kushughulikia suala la Zanzibar, ndivyo Waingereza nao walivyoonekana kupunguza kasi katika kushughulikia suala hilo.

Lakini huenda kujivuta kulitokana na kusubiri matokeo ya mazungumzo ya nchi tatu za Afrika Mashariki (Tanganyika, Kenya na Uganda) kuhusu kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki yaliyopangwa kufanyika mjini Nairobi kuanzia Ijumaa ya Aprili 10, 1964 na kumalizika siku iliyofuata.

Habari za kuanzishwa kwa shirikisho hilo ndiyo iliyoripotiwa katika toleo la kwanza la gazeti Nationalist and Freedom lilipotolewa kwa mara ya kwanza Aprili 17, 1964.

Mazungumzo ya kuanzishwa kwa shirikisho hilo yalimalizika bila maelewano. Karibu kila mtu aliyeshiriki katika mazungumzo hayo alionekana kuvunjika moyo.

Huenda viongozi wengine hawakuwa na nia ya kweli ya kuanzisha shirikisho hilo. Lakini ilibainika baada ya miezi minne kuwa mkutano wa Juni, 1963 wa kuanzisha shirikisho, “ulikuwa mbinu ya kuwahadaa Waingereza ili waharakishe kuipa Kenya uhuru”, kama alivyonukuliwa na Rais wa Kenya, Jomo Kenyatta katika kitabu cha Kenya: A History Since Independence kilichoandikwa na Charles Hornsby.

Katika ukurasa wa 102 wa kitabu hicho, Kenyatta anaonekana aliwahadaa pia hata Julius Nyerere na Milton Obote.

“Ingawa hadi mwaka 1965, Nyerere bado alikuwa anazungumzia shirikisho, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1964 wazo hilo lilikuwa limeshakufa.”

Inaelekea kuna mengi ambayo wajumbe katika mazungumzo hayo hawakuweza au hawakutaka kuelewana au kukubaliana. Lakini habari za gazeti hilo zilizotolewa siku saba baadaye zilisema “maofisa wa Kenya watetea shirikisho la Kenya, Tanganyika na Uganda.”

Inaelekea wakati mwingine Joseph Zuzarte Murumbi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alikuwa akifanya kazi kwa faida ya Marekani au Uingereza—pengine bila kutambua. Alikuwa akiwapa habari za mambo yaliyokuwa yakiendelea katika vikao vyao.

Mazungumzo ya kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki yalipomalizika katika hali ya kutoelewana, Joe Murumbi alituma taarifa kwa balozi wa Uingereza nchini Kenya, Geoffrey Stanley de Freitas ambaye ulituma ujumbe huo kwa balozi wa Marekani, William Attwood.

Ingawa mazungumzo hayo yalimalizika katika hali ya mvutano, taarifa ambayo Balozi Attwood aliituma Marekani ilisema, “Kwa mujibu wa (Joe) Murumbi, miongoni mwa mambo muhimu ya maana yaliyojitokeza katika mkutano huo ni mazungumzo ya pembeni na (Oscar) Kambona ambaye alikuwa na wasiwasi na kutishwa na athari za ukomunisti Zanzibar.

“Hali ya Zanzibar haikuzungumzwa sana na wala haikutoa mchango mkubwa, au tuseme mchango wowote, katika kuzikomboa nchi kubwa tatu (Tanganyika, Kenya na Uganda) na hakukuwa na mpango kwa Afrika Mashariki uliokuwa umeandaliwa ili kushughulikia jambo hilo,” ilisema taarifa ya Balozi Attwood.

Hili nalo linadokeza kwamba hata katika mkutano huo wa Nairobi, suala la Muungano wa Tanganyika-Zanzibar halikuguswa. Hilo nalo linadokeza kuwa mpaka wakati huo hakukuwa na wazo la muungano wa Tanganyika-Zanzibar.

Aprili 16, siku kumi kabla ya muungano, ndipo Serikali ya Zanzibar ilipotangaza kupiga marufuku uhamiaji, ikionya kuwa “hakuna mtu yeyote ambaye ataruhusiwa kuingia nchini (Zanzibar) isipokuwa kwa ruhusa maalumu ya Wizara ya Mambo ya Nje”.

Kwa mujibu wa gazeti la Tanu la Uhuru lililotoka Aprili 18, watalii walipigwa marufuku kufika Zanzibar “mpaka hapo taarifa zaidi itakapotolewa”.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi Visiwani, Sheikh Abdulrahman Mohammed Babu, ambaye alikuwa na wasiwasi na hata kuwachukia sana Wamarekani. Na moja kwa moja tangazo hilo liliwalenga Wamarekani.

Babu alitoa amri hiyo akiwa mjini Nairobi, Kenya na kusema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa makusudi kabisa kutokana na kuwapo kwa meli za kivita za Marekani katika pwani ya Afrika Mashariki.

Huenda meli hizo zilifika pwani ya Afrika Mashariki kutekeleza mpango wa kuivamia Zanzibar ulioitwa ZAP kama isingeungana na Tanganyika.

Haijulikani kama amri ya Babu ilikuwa ni pendekezo la Mwalimu Nyerere, uamuzi tu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au shinikizo kutoka nchi za Kikomunisti—hususan China.

Wakati Babu akitoa uamuzi huo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Oscar Kambona hakujua haraka kilichozungumzwa na Babu kwa sababu alikuwa katika mazungumzo na balozi wa Marekani ofisini kwake mjini Dar es Salaam.

Mazungumzo yao yalilenga moja kwa moja mpango wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar. Huko Zanzibar nako, Frank Carlucci kwa mara nyingine, alikuwa anakutana na Sheikh Thabiti Kombo kuhusu suala hilo hilo. Balozi Leonhart alijaribu kumshawishi Kambona, ili naye akamshawishi Nyerere na Karume kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Leonhart alimwambia Kambona kwamba kwa kuwa shirikisho la Afrika Mashariki limeshindikana, basi angalau kuwe na shirikisho la Tanganyika na Zanzibar. Kabla Kambona hajaondoka Nairobi kurejea Dar es Salaam na kukutana na Balozi Leonhart na Balozi Attwood, alimtumia Joe Murumbi ujumbe akimsihi amshawishi Kambona ili akamshawishi Nyerere. Kambona alielekea kushawishika.

Alipoondoka Nairobi, miongoni mwa wanadiplomasia wa mwisho kuagana nao alikuwa Attwood. Kambona alimuahidi mwanadiplomasia huyo kuwa angeshughulikia yale aliyomwambia.

Alimsisitiza kuwa ni kwa faida yake ikiwa atakutana na balozi wa Marekani nchini Tanganyika mara atakapowasili Dar es Salaam. Kambona alipofika Dar es Salaam alipanga kwenda kuonana na Leonhart. Isitoshe balozi huyo alikuwa akimsubiri Kambona kwa hamu kubwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa balozi mwenzake wa Nairobi.

Baada ya mazungumzo yake na Leonhart, Kambona alisisimkwa, na hata alipofika Ikulu ya Dar es Salaam alijaribu kumsisimua na Mwalimu Nyerere pia.

Itaendelea kesho