Waziri Mbarawa atoa maagizo kwa Dawasa, wakandarasi

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa

Muktasari:

  • Waziri wa Maji wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amewataka Dawasa na wakandarasi kuanza kazi mara moja baada ya kusainiwa kwa mikataba ya miradi sita mikubwa ya maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Dar es Salaam. Waziri wa Maji wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) na wakandarasi kutopoteza muda katika utekelezaji wa miradi sita ya uboreshaji wa huduma ya maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo, leo Jumanne Julai 2, 2019 wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba sita ya maji yenye thaman ya Sh114 bilioni hafla iliyofanyika ofisi za Dawasa, Gerezani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Dawasa, Davis Mwamunyange.

Miradi hiyo ambayo imeainiwa ni wa usambazaji maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo; Mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza; mradi wa kuendeleza visima vya Kimbiji na mradi wa usambazaji maji Kisarawe hadi Pugu (Gongolamboto, Pugu station, Airwing, Ukonga na Majohe).

Mingine ni; Mradi wa usambazaji maji katika mji wa Mkuranga na mwisho mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Mlandizi- Chalinze hadi Mboga

Profesa Mbarawa amesema sasa miradi inaanza kutekelezwa na hakuna muda wa kupoteza kwa kuwa watu wa mikoa hiyo wamesubiri maji kwa muda mrefu.

“Mradi ukianza kutekelezwa kila eneo ambalo miundombinu inajengwa tuwapelekee maji mara moja tusisubiri hadi mtandao wote ukamilike. Hatuwezi kusubiri mtandao ukamilike kwa mwaka mmoja na nusu haiwezekani, tukimaliza sehemu fulani tusafishe mabomba na tuwapelekea wananchi maji,” amesema Profesa Mbarawa.

“Tikifanya hivi kwa kila eneo Watanzania wataona matunda ya mradi huu.Lakini ule utaratibu wa kusubiri mradi kukamilika, hatutawatendea haki Watanzania, hilo siyo jambo geni Tabora tunafanya hivyo hivyo,” amesema Mbarawa.

Mbali na hilo, Profesa Mbarawa amesema kuna matatizo mawili katika wizara hiyo ambayo bado hayabadilika hasa kama mamlaka za maji, mojawapo ni makadirio ya juu ya miradi ya maji mbalimbali na mtandao huo unaanzia kwa wahandisi wa wilaya hadi wizarani.

“Kila mtu anataka kuchukua asilimia fulani, matokeo yake miradi imekuwa na makadirio ya juu,” amesema Profesa Mbarawa.