Waziri Mkuu amuonya DC Biharamulo, mkurugenzi kwa ushirikina

Muktasari:

Amesema kutokuelewana kwa viongozi hao ambao wakati mwingine wanatuhumiana kufanyiana vitendo vya kishirikina kumesababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo katika Wilaya hiyo

 

Kagera. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na mkurugenzi wa halmashauri hiyo,  Wende Ng’ahara wamalize tofauti zao na wasipojirekebisha atamshauri Rais John Magufuli  kufanya uamuzi mwingine dhidi yao.

Amesema kutokuelewana kwa viongozi hao ambao wakati mwingine wanatuhumiana kufanyiana vitendo vya kishirikina kumesababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo katika Wilaya hiyo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 20, 2019 wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mpira wa shule ya msingi Nyakanazi kijiji cha Nyakanazi, Biharamulo mkoani Kagera.

Amesema viongozi hao kutoelewana ni mfano mbaya kwa watumishi walio chini yao,  kuwataka kujirekebisha mara moja kwa kuwa wameaminiwa na Serikali kuliongoza eneo hilo na si kuwachanganya wananchi.

“Mliletwa hapa kuiwakilisha Serikali na kusimamia maendeleo ya wananchi nyie mnagombana.”

Awali, akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera alitembelea kambi ya Nyanza Roads inayojenga barabara ya Nyakanazi-Kabingo, inayounganisha Mkoa wa Kigoma na Kagera na kusema hajaridhishwa na kasi ya mkandarasi huyo.

Barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami ina urefu wa kilomita 50 na ilianza kujengwa mwaka 2014 ilitarajiwa kukamilika 2016, kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 60.