Waziri Mkuu apokea msaada vifaa vya mamilioni kutoka NMB

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Salum Tahir  (kushoto) ambaye ni  Mwenyekiti wa Taasisi ya Helping Hand kuhusu  vifaa mbalimbali vya hospitali  alivyokabidhiwa na Taasisi  hiyo kwa ajili ya hospitali, zahanati na vituo vya Afya wilayani Ruangwa. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye viwanja vya zahanati ya Nandagala leo Jumapili Julai 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa amepokea vifaa vya ujenzi wa zahanati kutoka Benki ya NMB vyenye thamani ya Sh25 milioni. Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 60, pia litakuwa na vyumba vya upasuaji.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumapili nJulai 28 amepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka benki ya NMB vyenye thamani ya Sh25 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, vifaa hivyo ni pamoja na fremu 46 za madirisha ya alminium na vioo vyake, milango 18, mabati 56, misumari na mbao, kompyuta 10 na madaftari 4050, vyote vikiwa na thamani ya sh25 milioni.

Jengo hilo jipya ambalo ujenzi wake umeanza, likikamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 60. Pia, kuna jengo lenye vyumba vya madaktari, vyumba vya upasuaji na vyumba vya kujifungulia.

Akipokea msaada huo leo kwenye zahanati ya Nandagala iliyopo wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu Majaliwa amewashukuru viongozi wa benki hiyo kwa kuamua kuchangia vifaa hivyo vya ujenzi.

“Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NMB kwa msaada huu mkubwa. Hii maana yake ni kwamba ni lazima tuharakishe kukamilisha jengohili ili tuanze kutoa huduma kwa wananchi wa Nandagala na wa vijiji vya jirani,” amesema.

“Tulianza na ujenzi wa zahanati kisha tukajenga jengo la upasuaji lenye wodi mbili. Moja ya wanaume na nyingine ya wanawake ambazo kila moja ina uwezo wa kulaza wagonjwa 20 kwa wakati mmoja,” amesema Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya msaada huo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali katika benki ya NMB, Vicky Bishubo amesema kipaumbele cha benki hiyo ni kutatua changamoto za afya na elimu kwa sababu sekta hizo ni nguzo kuu ya maendeleo kwa Taifa lolote.

“Vitu hivi tunavyokabidhi leo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na sisi kama benki inayoongoza Tanzania tunahakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayoipata,” amesema.

Amesema mwaka huu benki yake imetenga zaidi ya Sh1 bilioni kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu. “Mpaka ninavyoongea leo, tayari tumetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh600 millioni kwa mwaka huu tu,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nandagala, Andrew Chikongwe ameishukuru benki hiyo kwa kuwasaidia vifaa hivyo ambavyo alisema vimefika kwa wakati muafaka.

“Majengo yalikwishakamilika, yakabakia madirisha na milango, pamoja na vifaa tiba. Kwa hiyo sasa hivi tunaweza kuendelea na ujenzi,” amesema diwani huyo.