Waziri Mkuu apokewa na mabango, ampa mkurugenzi siku 15


Muktasari:

Wananchi wa Holili Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro leo Jumamosi Februari 23, 2019 wamempokea Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kero zinazowakabili.


Rombo. Wananchi wa Holili Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro leo Jumamosi Februari 23, 2019 wamempokea Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kero zinazowakabili.

Moja ya mabango hayo yanaeleza malalamiko yao kuhusu Halmashauri ya wilaya hiyo kushindwa kuwalipa wachimbaji wa madini ya Pozolana zaidi ya Sh114milioni.

Baada ya kuyaona mabango hayo, Majaliwa amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Magreth John kujibu madai hayo.

Mkurugenzi huyo alimueleza Waziri Mkuu kuwa  wananchi hao wanadai kiasi cha Sh12milioni  na si  Sh114milioni.

Majibu ya mkurugenzi huyo yaliwaibua wananchi na kuanza kumzomea na kumfanya Majaliwa kutoa siku 15 kwa Magreth kuhakikisha wananchi hao wanalipwa fedha zao.

"Mkurugenzi usibishane na mimi. Wananchi hawa wanadai zaidi ya Sh100milioni  na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha wanadai kiasi hicho cha fedha, zaidi ya Sh100milioni,"amesema Majaliwa

"Mkuu wa Mkoa naomba ulisimamie jambo hili la kuhakikisha wananchi wanalipwa fedha zao zote, na ukija Dodoma nipate hii taarifa ya malipo yao.”