Waziri Mpango akiri mkanganyiko wa sheria

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Serikali imekiri kuwepo na mkanganyiko kwa baadhi ya sera na sheria ambazo baadhi ya mikoa, wilaya na baadhi ya mamlaka za wilaya kutoheshimu mamlaka ya wizara

 

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango amekiri mkanganyiko wa sheria kwa taasisi zingine jambo alilosema ameshaagiza mamlaka husika kuangalia hilo.

Akihitimisha hoja ya hotuba yake bungeni leo Jumatatu Juni 3,2019, Waziri Mpango amekiri mkanganyiko wa sheria hizo kwa taasisi na mamlaka zingine.

Awali kamati ya bajeti ilikosoa mwingiliano wa sera za fedha na sera za kihasibu kuwa zimekuwa haziheshimu mamlaka za wizara.

Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki alisema jambo hilo limekuwa likipelekea baadhi ya tozo, ada na ushuru unaoanzishwa kuwa kero kwa wananchi na wafanyabiashara.

Waziri Mpango amesema tayari amewaandikia wahusika katika baadhi ya taasisi kuwakumbusha juu ya majukumu hayo.

Hata hivyo amesema utaratibu wa sheria na sera za tozo hujadiliwa na wizara na taasisi katika kipindi cha Desemba kila mwaka.