Waziri Mpango apendekeza utaratibu wa kuondoa mizigo bandarini

Wabunge wa Viti Maalum (Chadema) wakisoma kitabu cha hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ilipokuwa ikiwasilishwa bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango leo Alhamisi anawasilisha makadirio na mapato ya Serikali kwa mwaka 2019/20 ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia utaratibu utakaotumika kwa mwaka ujao wa fedha wa namna ya kuondoa mizigo bandarini


Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amependekeza kuweka utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida wataruhusiwa kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa Forodha.

Waziri Mpango amesema hayo wakati akiwasilisha makadirio na mapato ya Serikali kwa mwaka 2019/20 leo Alhamisi bungeni jijini Dodoma.

Huku akishangiliwa na wabunge, Waziri Mpango amesema licha ya kuweka utaratibu huo lakini, “hautahusisha mizigo inayopitishwa Tanzania kwenda nje ya nchi.”

“Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaandaa utaratibu wenye kueleweka kwa urahisi ili kuwawezesha Wananchi kugomboa mizigo yao kwa gharama nafuu zaidi na bila kuchelewa,” amesema