Waziri Mwinyi aridhishwa ujenzi nyumba za magereza, atoa maagizo kwa JKT

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Dk Hussein Mwinyi ( kushoto) akiwa na Kamanda wa Operesheni wa JKT, Brigedia  Jenerali Charles Mbuge wakikagua nyumba za askari na maofisa wa magereza leo.Picha Bakari Kiango.

Muktasari:

  • Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Tanzania, Dk Hussein Mwinyi amekagua ujenzi wa nyumba askari na maofisa wa magereza Ukonga, Dar es Salaam na kutoa maagizo agizo kwa JKT kuanzisha kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia ujenzi.

Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Tanzania, Dk Hussein Mwinyi ameagiza kuanzishwa kwa  kikosi  kazi kwa ajili kushughulikia ujenzi ndani ya JKT.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo, leo Jumatatu Julai Mosi, 2019 wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa nyumba za askari na maofisa wa magereza zinazojengwa eneo la gereza la Ukonga chini ya JKT.

Ujenzi wa nyumba hizo ulioanza Aprili, 2019 umefikia upo katika hatua ya umaliziaji baada ya Machi 16, 2019 JKT kukabidhiwa zabuni hiyo na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika nyumba hizo na kuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuachana na ujenzi huo baada ya kuonekana wanasuasua katika utekelezaji wake.

Akiwa eneo hilo la ujenzi, Dk Mwinyi ameelezea kufurahishwa, kuridhika na kasi, kiwango na fedha  Sh 1bilioni zilizotumika kati ya Sh5bilioni zilizopangwa kutekeleza mradi huo.

“Sasa hivi tunajivunia ndani ya JKT kuna vijana wenye kiwango kizuri  na uweledi kwenye jenzi. Tulikuwa na mpango kuanzisha kikosi kazi cha ujenzi, hatuoni sababu kwa nini tusifanye hivyo kutokana na idadi  ya mafundi waliokuwapo ndani ya JKT.

“Mtu yeyote ukimwambia hii kazi ilipofikia imejengwa kwa miezi miwili na nusu hatoamini lakini  vijana wa JKT wameifanya kama operesheni. Nampongeza  msimamizi wa ujenzi huu (Brigedia Jenerali Charles Mbuge ) kwa kazi nzuri, naondoka nikiwa nimeridhika na kazi hii,” amesema Dk Mwinyi.

 

Brigedia Jenerali Mbuge amesema walikabidhiwa kazi hiyo na Serikali ikiwa katika hatua ya nguzo, lakini ndani ya miezi miwili JKT imefanya kazi hiyo hadi kufikia kiwango cha umaliziaji wa majengo hayo yakatayo chukua familia 172 pindi yakikamilika.