Waziri Ndumbaro atoa somo kwa asasi za kiraia za SADC

Thursday August 15 2019

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Dk Damas Ndumbaro amezitaka asasi za kiraia za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kubeba ajenda ya viwanda inayohimizwa na jumuiya hiyo. 

Dk Ndumbaro aliyefungua mkutano wa asasi za kiraia za nchi za SADC zilizoanza mkutano wake jana Jumatano Agosti 14,2019 jijini Dar es Salaam kuwa daraja kati ya wananchi na Serikali za nchi za jumuiya hiyo.

“Ujumbe kutoka Serikali ni kwamba Rais John Magufuli anachukua uenyekiti wa SADC katika mwaka huu mmoja, tunawategemea azaki washirikiane na wabebe ajenda ya viwanda.

“Tunategemea sekta binafsi, azaki ziwe daraja kati ya wananchi katika nchi za SADC. Ziwe pia daraja kufikisha ujumbe na maoni ya wananchi kwa nchi za SADC,” alisema Dk Ndumbaro 

Huku akirejea kauli mbiu ya SADC ya mwaka 2019 inayosema. ‘Kuwa na mkakati jumuishi wenye kujali mazingira ya viwanda na kuongeza biashara kati ya nchi za SADC kwenye kutengeneza ajira kwa vijana,’ Dk Ndumbaro alizitaka asasi hizo kutetea nchi za jumuiya hiyo.

“Kama kuna nchi imewekewa vikwazo ni wananchi wanaoumia. Kuna Waafrika wanasafiri kwenda barani Ulaya wanapotea katika bahari ya Mediterranean, hili ni janga la Afrika. Kama wanadai haki za binadamu hizo ndio za kupigania,” alisema.

Advertisement

Wakizungumza baada ya ufunguzi kwa upande wa asasi za kiraia, baadhi ya wajumbe nao wamezitaka nchi za SADC kuzingatia haki za binadamu.

Ofisa uchechemuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Paulo Kanegene alisema licha ya kubeba ajenda hiyo wanazitaka nchi za SADC kuheshimu haki za binadamu ikiwa pamoja na haki za ajira kwa vijana na wanawake.

“Kwanza kauli mbiu ya mkutano wa SADC ya kuweka mazingira wezeshi ya viwanda na biashara, tunataka Serikali zetu zizingatie haki za binadamu. Tunajua kuna mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2012 uliotoa mwongozo wa haki za Binadamu katika biashara, huo unapaswa kuzingatiwa,” alisema Kanegene.

Aliendelea, “Katika viwanda tusisahau kilimo. Ni vizuri Serikali isimamie kilimo ili vijana wapate ajira. Tusikimbilie kwenye viwanda wakati kilimo bado. Tunaomba Serikali izingatie haki za vijana na wanawake katika ajira.”

Alitaja pia masuala ya ubaguzi ambayo alisema baadhi ya nchi za SADC limekuwa tatizo sugu na kuwa kikwazo cha ajira na biashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa asasi ya Tangible initiative for local development, Geline Fuko alizitaka nchi za SADC kuhakikisha uchumi wa viwanda unawagusa wananchi.

“Tunapoelekea kwenye viwanda ambayo ndio dhana ya SADC na ndio dhana ya Tanzania, kubwa kabisa uchumi huu unawafikia wananchi, uchumi jumuishi, uwafikie wanawake, vijana,” alisema Fuko.  

“Sisi kama mashirika yasiyo ya kiserikali kazi yetu ni kuikumbusha Serikali. Tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda lakini hatuna Mahakama inayoweza kuamua mambo ya viwanda. Inatakiwa pia wananchi wawezeshwe kufikia hizo fursa,” aliongeza.

Advertisement