VIDEO: Waziri Ummy alia taulo za kike kuuzwa kwa bei kubwa

Muktasari:

Wakati Serikali ya Tanzania ikiwa imeondoa kodi katika taulo za kike, imeelezwa kuwa bado zinauzwa kwa bei kubwa tofauti na ilivyotarajiwa


Dar es Salaam.  Wakati Serikali ya Tanzania ikiwa imeondoa kodi katika taulo za kike, imeelezwa kuwa bado zinauzwa kwa bei kubwa tofauti na ilivyotarajiwa.

Juni 14, 2018 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali mwaka 2018/19 alitangaza kufutwa kwa kodi hiyo.                                              Akizungumza leo Ijumaa Februari 15, 2019 wakati akifungua mkutano uliowakutanisha wadau wa elimu na masuala ya jinsia ukilenga kujadili namna ya kumkwamua mtoto wa kike kwenye kizingiti cha ndoa na mimba za utotoni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema bado taulo hizo zinauzwa kwa gharama kubwa hivyo lengo la kuwafikia walengwa halijatimia.

Kutokana na hali hiyo, Ummy amesema ameanza kuchukua hatua kwa kumuandikia barua Dk Mpango na Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda kuhusu sintofahamu hiyo.

 “Nimewaandikia waziri wa fedha na viwanda na biashara kuwataka waingizaji wa taulo za kike kupunguza bei ili kuhakikisha lengo la Serikali kuhakikisha wanawake wengi hasa wasichana walioko shuleni wanapata vifaa vya kujistiri kwa gharama nafuu, Sh2000 bado ni kubwa,” amesema Ummy.