Waziri afafanua kusogezwa mbele ujenzi barabara ya njia sita Dar-Chalinze

Wednesday May 15 2019

Waziri , kusogezwa ,mbele, ujenzi ,barabara,njia ,sita, Dar,Chalinze,

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imesogeza mbele ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 144 ili kukamilisha miradi mingine inayoendelea.

Hilo lilibainishwa wiki iliyopita na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alipokuwa anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao wa fedha, 2019/20.

Waziri Kamwelwe amesema kazi ya ujenzi wa barabara hii iliyopangwa kutekelezwa kwa expressway haijaanza kutokana na uamuzi wa Serikali kuisogeza mbele.

“Mradi huu unahusisha ukarabati kwa kiwango cha lami sehemu ya Mlandizi hadi Chalinze yenye kilomita 44 unaofanywa kwa awamu ambapo hadi Machi mkataba kwa ajili ya ukarabati wa kilomita 12.4 umesainiwa na maandalizi ya ukarabati yanaendelea,” alisema Kamwelwe.

Aidha, ujenzi wa barabara ya Kwa Mathias hadi Msangani yenye kilomita 8.3 kwa kiwango cha lami, waziri huyo amesema upo katika hatua za ununuzi au kumpata mkandarasi.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi hadi Ngerengere yenye kilomita 11 kwa kiwango cha lami, Kamwelwe ameeleza kuwa usanifu wake wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni umekamilika.

Ujenzi wa barabara hiyo inayokusudia kupunguza foleni katika Barabara ya Morogoro inayokuwapo zaidi kila asubuhi na jioni itakayokuwa ya kulipia, utaanzia jijini Dar es Salaam hadi Morogoro kupitia Chalinze.

Alipoombwa ufafanuzi na gazeti hili kuhusu kusitishwa kwa ujenzi wa barabara hiyo, waziri amesema kwa sasa Serikali inaitanua Barabara ya Morogoro itakayokuwa na na njia nane.

“Barabara itakuwa na njia nne za kwenda na nne za kurudi. Katikati kutakuwa na njia ya (mabasi ya mwendokasi) BRT hivyo zitakuwa 10. Tunaweza kuteua njia mbili kati ya hizo zikawa expressway,” alisema Kamwelwe.

Utekelezaji wa miradi ya ubia (PPP), inahitaji ushirikishaji wa taasisi nyingine za Serikali kwa kuwa mtekelezaji ni lazima alipwe na atakapolipwa maana yake atapunguza mapato ya Serikali.

Kwa kuwa malipo ya mbia atakayepatikana yatatokana na kodi za wananchi, ni lazima Hazina wajiridhishe na taarifa hizi ndizo zinazoenda hata Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.

“Bado kuna mazungumzo yanaendelea,” alisema.

Advertisement