Waziri alieleza Bunge muda wa mtumishi kukaimu

Naibu Waziri ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa akijibu maswali bungeni katika kikao cha 10 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetaja muda maalumu wa mtumishi kukaimu nafasi kuwa si zaidi ya miezi sita

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetaja muda maalumu wa mtumishi kukaimu nafasi kuwa isizidi miezi sita.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni Jumatatu Aprili 15, 2019 na Naibu Waziri ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Longido (CCM), Dk Steven Kiruswa

Hata hivyo, Mwanjelwa amesema mtu yeyote asipewe nafasi ya kukaimu hadi kibali maalumu kitolewe na watu wa utumishi baada ya kuombewa kibali.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itatoa vibali vya kuwathibitisha maofisa wanaokaimu wenye sifa za kukaimu.

Naibu Waziri ametoa kauli hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali Tanzania.

Amesema upungufu wa watumishi nchini hauna maana ya kuwapa nafasi wale wanaokaimu kwani mchakato wa kumthibitisha mtu hupitia mchakato mrefu.

"Serikali hufanya upekuzi wa watumishi wa umma wanaokaimu nafasi za madaraka ili kubaini iwapo wanafaa au la ambapo matokeo hutegemea upekuzi," amesema.

Kuhusu upungufu wa watumishi, amesema Serikali iko mbioni kuajiri watumishi 4,549 ambao watakuwa katika kada mbalimbali ambapo Longido imetengewa watumishi 177.