Waziri aliyefukuzwa na Magufuli ataja mambo 10 ‘yanayomtesa’

Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa gazeti la Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dodoma juzi. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Baada ya kufanya kazi kama Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miezi sita, Charles Kitwanga ametaja takriban mambo 10 ambayo alipanga kuyatekeleza, lakini muda haukutosha.

Hata hivyo, anashukuru kwani machache aliyoyasimamia ndani ya kipindi cha dhamana yake kuwahudumia Watanzania yalitekelezwa na yanatekelezwa, ikiwamo kuhakikisha haki na sheria zinasimamiwa.

Katika vita hiyo kwa kushirikiana na wataalamu, anasema walihakikisha wanavunja njia za kuingiza dawa za kulevya ili kuzuia zisiingie nchini na zilizokuwapo hazisambazwi kwa wananchi wala kwenda nje ya nchi.

“Tulikuwa hatutangazi sana lakini tulikuwa tunasema,” alisema Kitwanga, waziri wa Mambo ya Ndani wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya Tano katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, nyumbani kwake jijini hapa.

Kama angekuwa na muda mwingi zaidi ndani ya wizara hiyo, Kitwanga ambaye alifukuzwa uwaziri Mei 20, 2016 anasema alikuwa na malengo kwa kila jeshi na idara iliyopo kwenye wizara hiyo.

Anasema mtu hawezi kuwa na mipango ya leo tu na mara zote huwa anawaza leo, kesho, miaka 50 hata 100 ijayo. Kutokana na uwezo huo, anasema anamshukuru Mungu yu miongoni mwa watu wenye elimu wanaoweza kufikiri na kuweka mipango ya siku zijazo.

“Wizara ya Mambo ya Ndani ina watu makini sana, ni majeshi yanayokwenda kwa amri. Ni rahisi sana kufanya nao kazi,” anasema.

Anasema katika kila eneo alikuwa na mipango aliyotamani kuitekeleza. Kwa kutambua kwamba Serikali haina fedha za kutosha kufanikisha kila kitu, aliwashirikisha wataalamu kwa ajili ya miradi inayoweza kujifadhili.

Magereza

Katika mipango yake, Kitwanga anasema alikuwa anachukia kuiona Serikali bado inatoa chakula kwa wafungwa magerezani ilhali jeshi hilo linao wataalamu wa kilimo, viwanda na wengine wanaoweza kuweka mikakati ya kujitosheleza na kupata ziada.

“Ukijiuliza wengine wenye matrekta wanafayaje, ni ngumu kuelewa inakuwaje Magereza wanakosa vitu hivyo wakati wapo ndani ya Serikali tena wakiwa na maeneo makubwa yanayoweza kuwahakikishia dhamana ya mkopo wa vifaa vya kisasa,” anasema.

Polisi

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, anasema, “nachukia sare za khaki ambazo zipo tangu nikiwa mdogo na hazijawahi kubadilika.” Kitwanga amezaliwa mwaka 1960. Kutokana na hali hiyo, anasema wakati wa uongozi wake alikutana na viongozi wa jeshi hilo na kuwaambia wafikirie sare ambazo ni rafiki kwa raia, ambazo watazitumia kwenye mazingira ya amani na zinazobaki ziwe kwa ajili ya operesheni za kijeshi.

“Kuna yale makombati ndio siyapendi kabisa. Nikasema haya tuyavae tunapokuwa field lakini ziwepo sare zitakazotumika tunapokuwa kwenye kazi zinazoingiliana na raia. Naona trafiki wanawake wamebadilisha. Hata ukiwaona wanakuwa huru.”

Jingine, anasema ilikuwa ni kuboresha makazi ya askari kwa kutafuta namna ya kuwaweka pamoja kambini ili wakihitajika wapatikane kwa wakati.

Anasema kwa kuwa anaamini teknolojia inaweza kulikomboa jeshi hilo, alikuwa akiwaza kufunga taa za usalama (CCTV) katika jiji zima la Dar es Salaam, ambazo zingesaidia kudhibiti uhalifu na wanaovunja sheria ya usalama barabarani. Jiji la Nairobi, Kenya limefungwa kamera za aina hiyo.

Kitwanga anasema sehemu ya faini ambazo zingelipwa kwa msaada wa kamera hizo ingeenda polisi kusaidia kurudisha deni la mzabuni ambaye angezifunga. “Tulianza mipango ya kutafuta mtu atakayesaidia kufanikisha ufungaji,” anasema.

Zimamoto

Kutokana na ongezeko la nyumba za ghorofa, Kitwanga anasema Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kinahitaji zaidi teknolojia kukabiliana na majanga ya moto na kwamba, alipanga kuimarisha vituo vya maji.

Sambamba na vituo hivyo, alikusudia kuongeza idadi ya magari, yangekuwepo madogo na makubwa. Yale makubwa, anasema yangekuwa yanaegesgwa ofisini wakati madogo yakiwa mitaani kwenye vituo vilivyojengwa. Mpango huo ulikuwa umepangwa kuanza katika mikoa ya Dar es Salaam ambao ungekuwa na vituo vitatu pamoja na Arusha, Mbeya, Moshi, Zanzibar, Mwanza, Iringa na Morogoro.

Uhamiaji

Kwa sasa baadhi ya Watanzania wanamiliki pasipoti za kielektroniki zinazowaruhusu kutoka na kuingia nchini kwa malengo tofauti.

Kitwanga anasema matamanio yake ilikuwa kufahamu watu wote wanaoingia Tanzania kupitia mipaka yote iliyopo iwe Sirari au Horohoro, na alitaka kila anayeingia nchini aonekane ama ofisini kwa waziri au kwa kamishna wa uhamiaji. “Hili kama yalivyo mengine lingefanikishwa kwa teknolojia. Unaweza kutumia simu ya mkononi yenye mfumo uliofungwa kwenye vituo vyote. Simu sasa hivi inaweza kukuunganisha hata na mtu aliye Marekani, haishindikani kwa aliye Dar na popote Tanzania,” anasema.

“Tupo mbali sana kwenye kipengele hicho. Uhamiaji hawana mambo mengi sana, nilitaka mfumo utakaoonyesha nani anaingia Sirari na analipia kiasi gani hata siku nyingine tukimhitaji tunampata kwa urahisi.”

Kitwanga anasema, “haya yote sikuwa nayawaza kwa ajili ya kipindi changu tu, bali kuweka misingi ambayo hata watakaokuwepo miaka 50 ijayo wakubali kuwa kuna watu waliwaza ndio maana mambo yamekuwa mazuri.”